Menu

SAID ALHAJ ISSA:UDHAMINI NI KIKWAZO KWA MAENDELEO YA VOLLEYBALL YETU

Katika suala zima la kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana, nchi nyingi zilizoendelea zimekuwa zikijaribu kuboresha miundombinu kwenye kila sekta ili kutoa fursa kwa vijana kujipatia kipato na kuendesha maisha yao. Kwamfano kwa nchi yenye maendeleo makubwa ya viwanda kama China na Japan, tunategemea kuwa vijana wengi watapata ajira viwandani, na hilo lilikuwa ni lengo mojawapo la nchi hizo ili kumaliza kero ya ukosefu wa ajira. Hivyo ni lazima tukubaliane kuwa kila kero ina suluhisho lake.

Kwa nchi ambazo zimeendelea kwenye sekta ya michezo kama vile Brazil, Marekani, Urusi, China, Uingereza na nyingine nyingi, vijana wa nchi hizo wamekuwa wakinufaika katika suala zima la ajira wakiwa kama wachezaji, wajenzi wa viwanja, matabibu wa michezo, wauzaji wa vifaa vya michezo, watunzaji wa viwanja na kadhalika, lakini si vijana tu, bali hata wazee pia wananufaika ingawa vijana ndio sana kwa sababu karibu kila nchi, vijana ndio wengi kuliko rika jingine lolote.

Michezo sasa hivi ndio kila kitu katika dunia hii, na katika kulithibitisha hilo, ndio maana makampuni mengi ya kibiashara kama vile Cocacola, Pepsi, Fly Emirates na mengine mengi yamekuwa yakitumia michezo katika kutangaza bidhaa zao kwa kudhamini timu, mashindano, viwanja au hata kuingia mkataba na wachezaji maarufu kwa ajili ya kufanya nao matangazo ya bidhaa zao. Hii ni kwasababu michezo ina watu wengi wanaoifuatilia kwa ukaribu, watu ambao wapo radhi kuacha shughuli zao au kukatisha usingizi wao kwa ajili ya kuifuatilia.

Kwa hapa nchini Tanzania, michezo yetu inashindwa kupiga hatua kila kukicha sio kwasababu hatuna vipaji, ila ni kwasababu tunashindwa kuvitengenezea vipaji hivyo mazingira mazuri na salama katika uchezaji wao.
Said Alhaji Issa, ni mchezaji wa mchezo wa Volleyball anayechezea katika timu ya jeshi ijulikanayo kama CHUI, anawakilisha kundi hilo la vijana wa Kitanzania wenye vipaji vya hali ya juu katika michezo lakini wamekosa mazingira mazuri na salama ya kuonyesha vipaji vyao hivyo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 23 tu, ameanza kucheza Volleyball ya ushindani akiwa na klabu ya Tanzania Prison tangu mwaka 2012, baada ya kuzaliwa na kulelewa katika mazingira hayo ya Volleyball tangu alipokuwa shule ya msingi.

“ Vijana wa Kitanzania wenye vipaji katika Volleyball wapo wengi na wana uwezo wa kucheza hata nje ya nchi, lakini hawaandaliwi mazingira mazuri ya kuvikuza vipaji vyao katika utaratibu unaostahiki na mwisho wa siku huishia kucheza hivyohivyo tu bila ya kuwa na malengo”, Anasema Said.

Licha ya Said kuamini kuwa kuna vipaji vingi ndani ya Tanzania, lakini anakiri kuwa vipaji hivyo hususani katika mchezo wa Volleyball hupotea kwasababu hakuna misingi mizuri ya kuviendeleza kwani wao kama vijana wanahitaji kuwa na uhakika wa maisha yao kupitia ajira na uhakika huo wa ajira ni lazima utokane na Volleyball ili waweze kuifanya kama ni ajira kwao kitu ambacho kitawaongezea morali na bidii ili wasije kuipoteza ajira hiyo.

“Wachezaji wengi wa Volleyball Tanzania tunacheza Volleyball tu kwasababu tunaipenda lakini haitulipi, na ndio maana watu wanaamua kuichukulia Volleyball kama sehemu ya burudani tu huku wakitumia muda mwingi kujitafutia kipato kwa njia nyingine”, anaongeza Said.

Said anakiri kuwa yeye ni mojawapo ya wahanga wa suala la ajira kwa vijana ingawa anashangazwa na jinsi ambavyo kipaji chake kinashindwa kumletea suluhisho la tatizo hilo, na ndipo hapo anapoamua kueleza yake ya moyoni kuhusu nini kifanyike ili kuondoa hali hiyo.

“Ifike kipindi makampuni ya kibiashara na watu wenye uwezo wawekeze katika michezo mingine mbali na mpira wa miguu ili na sisi wengine tuweze kuonekana na kutimiza ndoto zetu kupitia vipaji vyetu tulivyopewa. Watu inabidi watambue kuwa si kila mtu atafanikiwa kutokana na elimu yake aliyonayo, ila kipaji pia kinaweza kumpa mafanikio, hivyo basi sekta ya michezo inabidi iangaliwe kwa jicho la tatu na makampuni ya kibishara ambayo ndio chachu ya maendeleo ya michezo kokote pale duniani”, Said anasisitiza.

Mzaliwa huyo wa tatu katika familia ya Marehemu Alhaji Issa anamaliza kwa kusema kuwa angependa kutimiza ndoto zake za kucheza Volleyball ya kulipwa kabla umri haujamtupa mkono, lakini anaamini kuwa hawezi kutimiza ndoto hiyo kama wahusika wa maendeleo ya michezo hawatafanya majukumu yao ipasavyo. Hivyo anayasisitiza makampuni ya kibiashara na watu wenye uwezo kuwekeza katika mchezo wa Volleyball kwa kudhamini mshindano mbalimbali, kumiliki timu za mchezo huo na hata kuvidhamini vyama vya mchezo huo hapa nchini ili viweze kuandaa mipango endelevu ya kuuendeleza mchezo huo.

Yaliyomo moyoni mwa Said Alhaji Issa yamesikika, tunaamini kuwa wahusika watafanya kazi yao ipasavyo kwa kushirikiana na serikali kupitia wizara ya michezo ili ifike wakati vipaji vilivyopo mtaani vitumike vyema kwa ajili ya kulitangaza taifa la Tanzania na kutoa fursa ya ajira kwa vijana

Soko la ajira limetawaliwa na wasomi, kama hujasoma huna chako,. Lakini njia mbadala ipo kwani tukitengeneza miundombinu mizuri ya michezo bila shaka vijana wetu wengi watapata ajira kupitia michezo kwani ukweli utabaki palepale kuwa vipaji tunavyo vingi sana.
Penye miti hapana wajenzi…!!!!

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets