Menu

NAMUONA JOSE MOURINHO NDANI YA JACKSON MAYANJA

Na Adam Mbwana,

Mayanja! Mayanja! Mayanja!……Kila ukinunua gazeti Mayanja…!, kila ukisikiliza kipindi cha michezo redioni ni Mayanja….!! Kila ukiangalia taarifa za habari za michezo ni Mayanja….!!! Huku kwenye mitandao ya kijamii ndio usiseme, Facebook ni Mayanja…!!, Twitter ni Mayanja..!! hadi Instagramuni ni yeye tu. Nahisi miongoni mwa watu maarufu kwa sasa Tanzania ni yeye, Magufuli, Diamond na Jecha.

Wiki chache zilizopita, Klabu ya Simba iliwasimamisha wachezaji wake wawili ingawa mmoja kashamaliza adhabu yake (Hassan Isihaka) huku mwingine akisubiria kamati ya nidhamu ya klabu hiyo ikae kumjadili. Wachezaji hao wanakabiliwa na utovu wa nidhamu kwa kocha wao Jackson Mayanja ambapo Isihaka alihoji kutopangwa mechi dhidi ya Yanga na Banda akigoma kupasha kwenye mechi dhidi ya Coastal Union.

Hilo sio suala la kushangaza sana maana ni kawaida tu, lakini kwa upande mwingine kuwajibishwa kwa nyota hawa kumemuongezea Mayanja umaarufu kwenye vyombo vya habari maana mara kwa mara amekuwa akikaririwa na vyombo hivyo akizungumzia suala hilo tena kwa kuweka msisitizo kuwa atasimamia nidhamu mwanzo mwisho na hatakubali mchezaji amdharau hata siku moja,

Ni kweli anachokisema Mayanja, wala hajakosea. Lakini kilichoniacha hoi mimi, na hapo jana nilipoona taarifa kwamba Mayanja amesema timu yake ya Simba inaweza kung’aa bila hata ya Banda kuwepo uwanjani hivyo wala hamnyimi usingizi kwasababu hakuwa mchezaji anayeanza kikosi cha kwanza mara kwa mara. Kauli hiyo ilinishtua na kunitoa macho kwani hivyo ni vijembe au watoto wa uswahili wanasema “Makavu Live”

Nilijiuliza maswali mawili juu ya tabia hii ya Mayanja kuwananga wachezaji wake kwenye vyombo vya habari mchana kweupe. Kwanza nikahisi labda Mayanja anataka kuwaonyesha wachezaji wengine kikosini kuwa hamuhusudu mtu, ukimzingua na yeye anakuzingua akiwa na lengo la kudumisha nidhamu, lakini pia nikahisi kuwa huenda Mayanja anataka kumkomesha Banda na kumuonyesha kuwa yeye ni zaidi yake na anaweza kumfanya chochote.

Kama hiyo haitoshi nikasikia kuwa Mayanja huyo huyo akiuzungumzia ujio wa Isihaka kikosini aliyemaliza adhabu yake kwa kusema kuwa sasa hivi Isihaka ana adabu na amekuwa mpole. Nikahisi Mayanja anataka kuuthibitishia umma kuwa mchezaji akipewa adhabu anarudi amenyooka.

Lakini kilichoniua zaidi ni pale niliposikia Mayanja huyohuyo akisema kuwa haogopi kusalitiwa na wachezaji wake kwasababu ya msimamo wake wa kusimamia suala la nidhamu, nikajiuliza ina maana Mayanja anataka kuwafuta mawazo wachezaji wenye malengo ya kuleta mgomo baridi Simba? Nikacheka kidogo, lakini kabla sijamaliza kucheka, nikakumbuka kuwa kuna mtu mwingine mwenye tabia kama hizi za Mayanja, sasa sijui nani amemuiga mwenzie maana sijajua nani alianza kazi hii ya Ukocha kabla ya mwenzie.

Nikamkumbuka mzee wangu Jose mourinho, mbwatukaji maarufu barani Ulaya na vitongoji vyake. Asiyeogopa mtu awe na ndevu za chuma au kamba, likimfika kooni analitapika tu na ndio maana aliporudi Uingereza kuinoa Chelsea kwa mara ya pili nikajua tu vyombo vya habari vitaneemeka kwa vichwa vya habari kama vile “ Mourinho aionya United”, na kweli bwana maana muda si muda nikasikia akimpa vidonge vyake mke wa Rafa Benitez aliyeongea ‘shit’ kuhusu Mourinho pale ambapo mumewe alikabidhiwa kibarua cha kuinoa Real Madrid. Mourinho hakumkawiza, alimpa kitu roho inapenda, lakini pia nikasikia Profesa Wenger naye akiitwa “Specialist of Failure” bila kusahau FA nao wakimegewa vipande vyao vya kutosha tu. Huyu ndiye Mourinho bwana

Mourinho hakukawizi, na wala haoni shida kumchana mchezaji wake kwenye vyombo vya habari. Utakumbuka aliporopoka kuwa anaamini kuwa Etoo amedanganya umri, lakini pia utakumbuka pale alipomchana Hazard kwa tabia yake ya kutosaidia timu kwenye ulinzi. Na hayo wala hayasemei dressing room, ni kwenye vyombo vya habari akiwa LIVE bila chenga. Na kubwa zaidi ni pale alipoliita jopo la madaktari la timu hiyo likiongozwa na Eva Corneiro kuwa ni wajinga wasiojua mambo kwa kuingia kumtibu Hazard wakati mechi inaendelea.

Kilichomkuta Mourinho sote tunakijua, sasa hivi yupo zake anakula good time akiivizia United itangaze dau baada ya kutimuliwa Chelsea. Nahisi mdomo ulimponza Mourinho kwasababu kitendo cha kuwachana wachezaji wake mbele ya vyombo vya habari kiasi kile ni sawa na kuwadhalilisha kwani wangeweza kumalizana ofisini tu. Mwisho wa siku akawaita wasaliti kwa kitendo cha kufungwa mfululizo akidai kuwa wachezaji walimchezea fitina. Labda inawezekana waliamua kumtumbua maana alishakuwa jipu sasa.

Sio vibaya kueleza hisia zako juu ya jambo linalokukera, lakini kuna vitu ukiwa kama kocha hutakiwi kuwapa faida watu wa nje, maana waandishi wa habari kwa kukoleza habari tu hawajambo. Unaweza kuwaambia timu yangu ilicheza vibaya leo, wao wakaenda kuandika kuwa kocha awalalamikia wachezaji. Simaanishi kuwa hawajui wanachokifanya, Lahasha! Ila chumvi zimezidi.

Mdomo wa Mourinho nauona umetua Airport ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na sasa anao Mayanja anazunguka nao. Kuwasema wachezaji vibaya mbele ya waandishi wa habari hata kama wana makosa sio vizuri kwani inawawekea kinyongo juu yako na mwishowe wakuchukie bureee maana nao ni binadamu na wana mioyo ya nyama. Hata kama hawatadhamiria kucheza chini ya kiwango, lakini wanaweza kufanya hivyo kwa bahati mbaya maana ulishawaharibu kisaikolojia kwa kuwaonyesha kuwa wewe ni zaidi yao. Ni sawa kufanya hivyo lakini isiwe kwa kutumia maneno makali kama hayo Mayanja aliyoyasema juu ya Banda hata kama mchezaji ana kiburi au anajisikia sana.

Mourinho na Mayanja wana sifa mbili zinazofanana, kwanza wanapenda ‘attention’ ya vyombo vya habari na pili hawaoni shida kumbwatukia mtu anayewakera hadharani. Sasa Mayanja aangalie yasije kumkuta waliyomkuta pacha wake, Mourinho maana nahisi Mourinho mdomo wake ulimponza mpaka akapoteza kazi maana siamini kama Diego Costa alikuwa anakosa magoli ya wazi kiasi kile wakati kwa sasa chini ya Hiddink anatupia atakavyo.

Siwashawishi Simba wafanye hivyo, Lashasha! Ila lengo langu ni kutaka kuona wachezaji na makocha wanatunziana heshima ili waweze kufanya kazi kwa pamoja maana watu hawa wanategemeana.

Mayanjaaa……!!! Wewe ni Mourinho wa bongo? Nijibu tafadhali.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets