Menu

KESSY: MSAMEHE MANARA BURE AU UKALALE KORIDONI MAANA VYUMBA VIMEJAA  

 

Na Adam Mbwana,

Wakati ulimwengu wa wapenda tamthilia ukisubiria misimu mipya ya tamthilia maarufu kama vile Game of Thrones, Avatar, Vikings na hata zile za bongo movie, mimi akili yangu haipo huko kwani uhusika wa Jon Snow kwenye Game of Throne hauniumizi kichwa kabisa bali nimetega masikio kusikia tamthilia inayomhusu beki wa kulia, Hassan Ramadhan Kessy na klabu yake ya Simba. Huenda hiyo ikawa ni tamthilia ambayo mwendelezo wake upo mbioni kukamilika.

Ikiwa ni miezi mitatu tu tangu kusajiliwa kwa mchezaji huyo kutoka klabu ya Mtibwa Sugar katika dirisha dogo la mwezi Desemba mwaka 2014, Hassan Kessy alianza kushikana mashati na waajiri wake hao baada ya kugoma kujiunga na kikosi hicho kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar huko Kambarage Shinyanga ambapo alidai kuwa uongozi wa Simba ulikiuka mkataba kwa kutommalizia kiasi cha pesa ya usajili ikidaiwa kuwa ni milioni 10 na kutompa nyumba ya kuishi kama waliyomuahidi.

April mwaka jana nikasikia kwamba Kessy alisema hana furaha kutokana na kuishi kwenye makazi ya wenzake kwani yeye hana makazi maalumu ambayo Simba waliahidi kuwa watampa mchezaji huyo aliyesajiliwa kwa kitita cha Milioni 30 za Kitanzania kwa mkataba wa miezi 18. Tamthilia iliendelea kwa msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara kudai kuwa Kessy hajaungana na wenzake kutokana na matatizo ya kifamilia lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na mchezaji huyo ambaye alidai kuwa ana madai na Simba na si kwamba ana matatizo ya kifamilia.

April hiyohiyo wiki mbili baadaye, nikasikia tena kuwa Kessy na Simba wamemalizana huku Manara akijinasibu kuwa hakuna taasisi isiyodaiwa kwahiyo wamemlipa Kessy pesa ya kulipia nyumba kama walivyomuahidi hivyo mchezaji huyo amejiunga na wenzake kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbeya City

Wakati dirisha dogo la usajili likiwa linakaribia, Novemba mwaka jana, Kulianza kuwa na fununu kuwa Kessy anatakiwa na vilabu vya Yanga na Azam ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu mchezaji huyo ajiunge na Simba, shukrani kwa Azam walioamua kubaki kimya lakini Yanga wenyewe kupitia kwa aliyekuwa katibu Mkuu wao, Jonas Tiboroha, waliamua kukata mzizi wa fitina baada ya kusema wazi kuwa hawana mpango wa kumsajili ‘mtoto’ huyo kama ambavyo Tiboroha alimuita na Tiboroha akaenda mbali zaidi na kusema kuwa wanaozusha taarifa hizo wanataka kumpa umaarufu ‘mtoto’ huyo ili aongezewe mkataba na timu yake ya Simba.

Sasa tangu fununu hizo za Kessy kwenda Yanga au Azam ziishe, kumekuwa na utulivu kati ya Kessy na Simba mpaka hapo mwishoni mwa juma hili lilipotokea la kutokea. Kessy alipigwa na kipa wa Simba raia wa Ivory Coast, Vicent Agban kwa madai kuwa mchezaji huyo ameifungisha makusudi timu hiyo baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumkanyaga Christopher Edward wa Toto Africa hali iliyopelekea kufungwa katika mchezo huo, lakini pia kumekuwa na tuhuma za chinichini za beki huyo wa kulia kuihujumu timu yake hiyo kwenye mchezo na watani zao wa jadi, Yanga ambapo Kessy alitoa pasi fupi kwa kipa iliyonaswa na Donald Ngoma aliyefunga bao la kwanza.

Tuhuma hizo za hujuma ziliendelewa kuchochewa kuni baada ya beki huyo kuanza kuwekwa benchi na Mayanja hali iliyofanya watu waamini kuwa kuna kitu kinaendelea chinichini

Kilichonishangaza hapo juzi ni pale niliposikia klabu ya Simba imesema wazi kuwa beki huyo wa kulia kama anataka kuondoka basi aende wala hawatambembeleza kwa maana walikuwepo wachezaji wazuri Simba na wakapita. Kisa cha Haji Manara kujawa povu na kutamka maneno hayo ni kutokana na kuenea kwa ubuyu kuwa Kessy amesema hawezi kuendelea kuichezea Simba baada ya kupigwa na Agban kwenye mchezo dhidi ya Toto. Hapo ndipo msimu mpya wa tamthilia hii ndefu ambayo ilitulia kwa muda inapoanza tena.

Sina hakika kama ni kweli Kessy amesema hayo maneno, lakini pia sina uhakika kama Manara amekurupuka kutoa kauli hiyo nzito bila kuwa na uhakika kwasababu kwa maelezo yake tu, anaonyesha kuwa hana uhakika kama Kessy amesema au hajasema, na hata kama Kessy hajatoa kauli hiyo basi pia kutakuwa na tatizo maana kashapigwa dongo ambalo haliwezi kufutika akilini mwake ya kwamba yeye ni wa kupita tu kwahiyo hawezi kuwababaisha.

Lakini kama waswahili wanavyosema kuwa lisemwalo lipo na kama halipo laja, basi mimi binafsi nitumie fursa hii kumwambia Kessy kuwa vyumba vimejaa. Najua kutokana na kiwango chake alicho nacho kwa sasa ni dhahiri shahiri kuwa mchezaji huyo atakuwa ameshapewa ahadi mbili tatu huko nje kuwa atasajiliwa kama ilivyokuwa kwa wenzake waliomtangulia.

Ukitoka Simba basi daraja linalofuata ni Yanga na Azam, na ukiangalia huko Yanga na Azam ambao ndio wahusika wakubwa wa Kessy, kumejaa na wala hakuna chumba kilicho wazi kwa ajili yake. Azam wana kapombe ambaye sote tunaujua uwezo wake. Beki wa kulia mwenye magoli sawa na washambuliaji wa timu hiyo na tangu kuumwa kwake, Azam imekuwa ikapata matokeo ya kusuasua bila kusahau kuwa Mkwasa anamtegemea pia katika kikosi cha Taifa Stars. Lakini pia huko Yangakuna Juma Abdul, beki wa kulia anayepiga mipira iliyokufa kama kachanjiwa, lakini pia amesha-fit kwenye mfumo wa Pluijm na si rahisi kumpokonya namba.

Naujua uwezo wa Kessy kuwa ni mkubwa lakini huko anapopaota yeye kwa sasa ni pagumu na vyumba vimejaa, na endapo akienda huko basi benchi linamhusu kwa asilimia mia moja kitu ambacho kitamharibia kiwango chake tena katika umri wake mdogo. Labda kama aseme anataka kurudi kwenye daraja alilotoka ambapo atacheza kila siku isipokuwa tu hatutapata nafasi ya kumuona wala kumsikia mara kwa mara.

Ifike kipindi Kessy aache kuchukulia maisha yake kihasira hasira. Kama alikuwa anatafuta sababu ya kukimbia Simba basi ajue kuwa huko anapotaka kwenda ni kugumu maana kuna watu kama yeye au zaidi yake. Huu ndio umri wa yeye kukuza kiwango chake pale alipo ili ajisogeze mbele zaidi na si kuingia kwenye malumbano na uongozi wa klabu hiyo pasi sababu ya msingi maana mwisho wa siku Simba itaendelea kubaki vile vile na yeye ndiye ataathirika zaidi.

Kama kweli hajatamka maneno hayo, basi amsamehe Manara bure ili maisha yasonge kwani kauli zile za Manara zinahitaji kifua kipana, lakini kama kweli amesema, basi anajifungulia milango ya kutoka pasi kujua kuwa huko afikiriapo kwenda, vyumba vimejaa labda akalale kwenye Korido.

Tusubiri msimu mpya wa tamthilia hii utakavyokuwa ili kujua hatma ya mhusika mkuu, Hassan Kessy.

Ni maoni yangu tu.

 

 

 

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets