Gareth Bale ameendelea kuwa chachu na moyo wa mafanikio ya Wales katika michuano ya Euro inayoendelea nchini Ufaransa.

Baada ya kufunga dhidi ya Slovakia na Uingereza katika mechi zake mbili za awali Euro 2016, mshambuliaji huyo wa Real Madrid alitupia goli lake la tatu katika michuano kikosi cha Chris Coleman kikiifungasha virago Urusi kwa kipigo cha 3-0 katika mechi za kumaliza hatua ya makundi wakimaliza kileleni mwa kundi B Jumatatu.

Kwa kufanya hivyo, Bale amevunja rekodi ya miaka 58 kwani amempiku Ivor Allchurch kuwa mfungaji wa muda wote wa nchi yake kwenye michuano mikubwa.

Si Bale pekee aliyeweka historia ya nchi yake lakini mwanzo wake mzuri unamweka katika mtazamo wa kipekee kwenye michuano hiyo. Akifunga katika kila mechi ya hatua ya makundi ni mafanikio yasiyo na ubishi – na hakuna hata mmoja katika michuano miwili iliyopita aliyefanikiwa kufanya hivyo.

Mwanzo maridadi wa Bale kwenye fainali za 2016 ni jambo ambalo hatujawahi kuona tangu enzi za Milan Baros wa Jamhuri ya Czech na Ruud van Nistelrooy wa Uholanzi waliofunga mechi zote tatu katika hatua ya makundi ya Euro 2004.