Menu

KAMA SHERIA NI MSUMENO BASI WANAPOFUNGIWA WAHUJUMU MATOKEO WASISAHAULIKE NA WAHUJUMU MAPATO PIA

 

Na Adam Mbwana,

“Muda mwingine kuna makosa lakini tunapocheza vizuri basi ujue mashambulizi yameanzia kwa golikipa. Ni vigumu kucheza na Barcelona ukiwa na wachezaji 11, kwahiyo kubaki 10 uwanjani tayari mechi ilikuwa ni kama imeisha tu”

-Pep Guardiola

 

Haya yalikuwa ni maneno ya Pep Guardiola, kocha wa Manchester City ambaye ni miongoni mwa makocha bora kabisa duniani kwa sasa. Guardiola aliongea maneno hayo baada ya Manchester City yake kupokea kichapo kizito cha mabao 4-0 dhidi ya Barcelona kwenye mchezo wa Ligi ya mabingwa barani Ulaya huku golikipa wake, Claudio Bravo akifanya makosa ya kizembe kabisa ambayo yaliigharimu timu kwa yeye kupewa kadi nyekundu na kutolewa nje hali iliyoifanya City kucheza pungufu.

Lakini kwa wale wafuatiliaji wa Ligi Kuu ya Uingereza, tutakumbuka jinsi ambavyo mlinzi wa Chelsea, Gary Cahill ‘alichomesha’ kwenye mechi mbili za ligi za hivi karibuni ambazo Chelsea walishindwa kupata matokeo. Septemba 11 kwenye mchezo dhidi ya Swansea alifanya makosa ya kushindwa kuumiliki mpira akiwa peke yake na kumruhuru Leroy Fer kuchukua mpira na kwenda kufunga goli laini kabisa mechi ikiisha kwa sare ya 2-2, lakini pia Septemba 24 akifanya makosa yaleyale baada ya kupiga pasi fupi kwa kipa iliyonaswa na Alexis Sanchez aliyeenda kufunga goli laini huku Chelsea ikifumuliwa mabao 3-0.

Tuendelee na mada yetu kwanza halafu utaelewa huko mbele nilikuwa namaanisha nini kuanza na mifano hii.

Tangu Kagera Sugar apokee kichapo ‘heavy’ cha mabao 6-2 kutoka kwa Yanga Oktoba 22 kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, nimekuwa nikisubiria kwa hamu kujua Uongozi wa Kagera Sugar utayapokeaje matokeo hayo ya ‘kushtukiza’ kama ambavyo wengi wameyaita.

Siku zote hizi ambazo viongozi wa timu hiyo walikuwa kimya nilihisi huenda lile jinamizi linaloitwa HUJUMA limeshapita na taratibu nilianza kutabasamu nikijua ukomavu wa soka umeshawaingia viongozi wetu lakini nasikitika kusema kuwa nilichokuwa nakitegemea sivyo kilivyo kwani baada ya siku sita kupita tangu Kagera Sugar wale kichapo hicho kizito, Hatimaye Uongozi wa klabu hiyo umeyatoa makucha yake nje na kuwasimamisha wachezaji wawili kwa tuhuma za kuihujumu timu kwenye mchezo huo.

Wachezaji hao ambao ni mlinda mlango Hussein Sharifu ‘Casillas’ ambaye inadaiwa alifungwa magoli ya kizembe ambayo hayakustahili kuwa magoli huku naye mlinzi Erick Kyaruzi akidaiwa kufungisha goli kwa makusudi na wachezaji hao wamewekwa kando kwa muda usiojulikana ili kupisha ‘uchunguzi’

erick

Erick Kyaruzi

Nianze kwa kusema kuwa kuna vitu vinasikitisha kwenye soka la Tanzania na kama hakutakuwa na jitihada za kuvimaliza vitu hivi basi hatutakaa tupige hatua.

Kuna vitu vikubwa viwili watanzania wapenda soka tunavikosa. Kwanza ni Subira na pili ni Kukubali kushindwa. Tunakosa subira kwa maana ya kwamba wengi wetu tunadhani matunda ya soka hupatikana ndani ya muda mfupi tena kwa magumashi magumashi yetu haya haya na hatukubali kushindwa hata kama tulistahili kushindwa.

Tunaposhindwa huwa kuna visingizio kede kede. Utasikia mchezaji fulani kahongwa hela na wapinzani ili afungishe, utasikia waamuzi wamehongwa hela ili wapendelee timu fulani, tena na wengine huenda mbali zaidi wakisema kuwa TFF ina timu zao ambazo inataka zichukue ubingwa.

Nisiwe mnafiki, mimi binafsi niliposikia Kagera Sugar kafungwa magoli 6-2 nilistaajabu na sikuamini kirahisi lakini nilipokuja kutaarifiwa kuwa wachezaji walisafiri kwa basi kwenda Kagera kutokea Pwani walipokuwa wakicheza mchezo dhidi ya JKT Ruvu siku tatu kabla ya mchezo dhidi ya Yanga wala sikushangaa tena maana safari ya Kagera sio mchezo hasa ukiwa unatokea ukanda wa mashariki tena hapo hukupata hata muda mrefu wa kupumzika wakati unaenda kupambana na Yanga ambao walishatangulia huko wanakusubiri, nikajua ilikuwa ni halali yao kufungwa kwa idadi ile ya magoli.

umbali

Umbali kutoka Dar es Salaam hadi Kagera ambao ni sawa na Kilometa 1008 walizosafiri wachezaji wa Kagera Sugar kwenda kuivaa Yanga

Sitaki kusema kwa uhakika kuwa Casillas na Kyaruzi wanaonewa, lakini naangalia chanzo cha tatizo haswa. Timu inapokuwa inafungwa hususani na timu kubwa zenye kipato angalau cha juu kama vile Simba, yanga au Azam basi ni lazima tu itakuwa na kisingizio kuwa ilionewa au kuna wachezaji wao walihongwa. Inawezekana ikawa kweli wala sikatai lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda tuhuma hizo zinazidi kuwa nyingi kwenye soka letu na zinaharibu maana halisi ya neno Ushindi.

Najaribu kuangalia sababu za wachezaji kukubali kuhongwa pesa na timu pinzani ili wazifungishe timu zao kwenye mechi dhidi ya hizi timu kubwa. (kama ni kweli vitendo hivyo vipo).

Nagundua kuwa sababu ya kwanza ni mishahara midogo- wachezaji wa timu hizi za kawaida ukiacha Simba, Yanga na Azam wanalipwa mishahara midogo sana ambayo haikidhi haja zao katika kukabiliana na maisha ya sasa na hiyo husababishwa na vilabu vyao kutokuwa na vyanzo vya mapato vya kutosha. Katika hali ya kawaida mchezaji lazima ashawishike kupokea kitita cha pesa ili afungishe kwani hata huko maofisini tunaona wafanyakazi wanawaibia mabosi wao pesa.

Sisemi kuwa kitendo hicho ni halali eti kwasababu hawalipwi vizuri, lakini tukumbuke kuwa wao nao ni binadamu na wanahitaji kuishi. Kama kweli wanafanya vitendo hivyo basi ni lazima kuna sababu mama ambavyo ndiyo inabidi itatuliwe ili mfumo mzima wa timu uweze kuwa salama.

casillas

Hussein Sharif “Casillas”

Kama mchezaji analipwa kiasi kidogo cha pesa tena pesa hiyo hailipwi kwa wakati muafaka na ana familia anaitunza unategemea nini? Kama klabu haina vyanzo vya mapato vya kueleweka zaidi ya kutegemea pesa za viingilio, ada za wanachama ambao hawafiki hata elfu moja na udhamini wa ligi kutoka Vodacom tu unategemea nini? Kama klabu ina viongozi ambao wanategemea kushibisha matumbo yao kwa kutumia pesa za klabu unategemea nini? Unategemea itasafirisha wachezaji wake kwa ndege ili kuwapa nafasi ya kupumzika kuelekea mchezo unaofuata? Unategemea itawalipa mishahara mikubwa wachezaji wake tena kwa wakati muafaka? Unategemea itasajili wachezaji wenye viwango vya juu wa kuwawezesha kushindana na kutwaa mataji? Lahasha! Labda kwenye Bongo Movie tu ndio ingewezekana.

Sio kwamba Simba, Yanga na Azam ndio wanafanya vyote hivyo kwa wakati, lakini angalau naweza kusema kuwa wanajitahidi kufanya hivyo kutokana na kuwa na kijipato kizuri angalau kwani waswahili wanasema kuwa; Kwenye nchi ya vipofu, mwenye chongo ndie kiongozi wa wenzie.

Ifike kipindi tuache kuwapaka matope wachezaji kwasababu ya makosa ya viongozi wenyewe. Suala la kulalamika kuhujumiwa na wachezaji au kulalamikia waamuzi imekuwa ni ‘fashion’ siku hizi kwenye VPL kwani humo ndimo viongozi hupatia vichaka vya kufichia maovu yao.

Mara nyingi Julio amekuwa akilalamika kuwa waamuzi wanaionea Mwadui FC mpaka kufikia hatua ya kujiuzulu huku akisema kuwa kitendo cha waamuzi kuzipendelea klabu kubwa za Yanga na Azam ndio kinafanya klabu hizo zisifanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

Napingana na kauli hiyo ya Julio kwa mantiki moja  tu kuwa: Yanga na Azam zinaweza kuwa zinafanya vizuri kwenye ligi ya ndani kwasababu zinacheza na ‘wachovu’ kwa maana ya kuwa zinacheza na timu ambazo haziwahudumii wachezaji wake ipasavyo na wala hazina kipato cha kununua wachezaji bora na kuajiri benchi bora la ufundi. Hakuna mtu aliyewahi kulifikiria hilo lakini badala yake kila mtu anasema kuwa timu hizo kubwa zinahonga wachezaji wa timu pinzani ili zipate matokeo. Huo ni ufinyu wa fikra! Haya sasa Julio kaondoka, Mwadui imeanza kupata matokeo na kutoka mkiani mwa ligi. Au marefa walikuwa hawampendi Julio tu?

Ilinifurahisha kauli ya kocha wa Singida United Fredy Felix Minziro ambaye aliamua ‘kumchana’ ukweli kocha wa Polisi Dodoma. Polisi Dodoma ilifungwa kwa mabao 2-0 na Singida United kwenye mchezo wa ligi daraja ya kwanza wiki moja iliyopita. Kocha wa Polisi alipohojiwa na waandishi alidai kuwa maamuzi ya refa ndio yamewaponza. Lakini Minziro alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo alimwambia kocha mwezie huyo kuwa aache kulalamika na badala yake aandae timu yake vizuri. Minziro alisema kuwa Polisi Dodoma haikufanya usajili mzuri na wachezaji wake wanaonekana wana uchovu ndio maana wameshindwa kupata ushindi. Alichokisema Minziro ndio kina mashiko na sio kuwatuhumu wachezaji pekee.

Fred Felix Minziro, Kocha wa Singida United

Fred Felix Minziro, Kocha wa Singida United

Ifike kipindi tusiangalie sababu za nje ya uwanja pekee pale inapotokea tumeshindwa kupata matokeo mbele ya hizi timu ‘kubwa’. Kuna sababu za ndani ya uwanja (technical) ambazo hakuna anaezizungumzia kama vile ubora wa wachezaji na benchi la ufundi, uchovu, mazingira ya kufanyia kazi na saikolojia nzima ya mchezaji kuelekea kwenye mechi.

Timu ndogo zijaribu kupunguza ‘gap’ kati yao na hivi vilabu vikubwa ili kupunguza lawama za kuonewa na waamuzi na kuhujumiwa na wachezaji wao. Waongeze vyanzo vya mapato ili waweze kusajili wachezaji bora na kuwalipa mishahara minono itakayowafanya wasishawishike na rushwa, lakini pia wawajengee mazingira mazuri wachezaji wao ili wafanye kazi yao kwa ufanisi weredi mkubwa na viongozi waache tamaa zisizo na msingi.

Kwa ‘maboko’ yale aliyotoa Gary Cahill kwenye mechi ya Swansea na Arsenal ingekuwa ni bongo basi angeshafukuzwa kwenye timu moja kwa moja, na kwa ‘kuchomesha’ kule kwa Claudio Bravo kwenye mechi dhidi ya Barcelona na Manchester United basi angewekwa benchi milele. Lakini kwasababu kule ni Ulaya na hapa ni Tanzania basi Hussen Sharif na Erick Kyaruzi kazi wanayo.

Sijui uchunguzi ukikamilika wakaonekana hawakuwa na hatia itakuwaje?

Najaribu kufikiria kwa sauti.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets