Menu

MWAROBAINI MMOJA WA CONTE UMETIBU MAGONJWA MANNE SUGU KWENYE KIKOSI CHA CHELSEA

Na Adam Mbwana,

Nakumbuka siku ya tarehe 26 mwezi Septemba mwaka huu huku zikiwa zimepita siku mbili tu tangu Chelsea ipokee kichapo cha haja cha mabao 3-0 kutoka kwa Arsenal niliandika makala ambayo nilibainisha matatizo manne makubwa yanayoikumba Chelsea ya Antonio Conte, Chelsea ambayo siku hiyo ilicheza vibaya na kwa uchovu wa hali ya juu.

Moja ya mambo ambayo niliyazungumzia ni pamoja na kitendo cha Antonio Conte cha kucheka na Cahill na mwenzake Ivanovic ambao walionekana kutokuwa na msaada kwenye timu hususani kwenye nafasi ya ulinzi hasa baada ya Gary Cahill kutoa maboko mawili mfululizo kwenye mechi dhidi ya Swansea akimpa Leroy Fer goli la ofa Chelsea ikipata sare ya bao 2-2 kwenye dimba la Liberty Stadium huku siku chache baadae akimzawadia Alexis Sanchez goli la bure bure na kuifanya Chelsea kufa kifo cha mbwa mwizi.

Lakini pia sikuona sababu ya kutompa ‘Makavu Live’ David Luiz kuwa ujio wake kwenye kikosi haukuwa wenye msaada kwa kitendo chake cha kubutua mipira mbele hali iliyokuwa ikiifanya Chelsea kushindwa kucheza kwa utaratibu maalum huku safu ya kiungo ya timu hiyo ikionekana kupwaya hususani kwenye mchezo dhidi ya Arsenal.

Sikuishia hapo tu, kwani nilienda mbali zaidi kwa kutabiri kuwa kama Eden Hazard akiendelea kucheza kama alivyocheza siku ile kwa staili yake ya kupiga pasi nyuma badala ya kwenda mbele basi asahau kuwa mchezaji wa kiwango cha dunia huku nikimalizia na Thibaut Courtois ambaye alikuwa akionekana kucheza ili muda uishe amalize aondoke huku nikiukumbuka uzalendo wa mkongwe Petr Cech.

Siwezi kusema kuwa Conte alinisikia kwasababu najua haelewi lugha ya Kiswahili lakini naamini kuwa mambo niliyoyaainisha siku ile ndiyo ambayo yalikuwa yakimuumiza kichwa akitafuta njia sahihi ya kuyatibu matatizo hayo kwa muda mfupi bila ya kupoteza mwelekeo.

Chelsea ilianza msimu ikitumia mfumo wa 4-1-4-1 ambao ulikuwa na walinzi wanne, (Cahill, Terry, Ivanovic na Azpiliqueta), ikiwa na kiungo mkabaji mmoja (Kante) Viungo washambuliaji wanne (Matic, Hazard, Willian na Oscar) huku ikimsimamisha Diego Costa mbele. Mfumo huu ulionekana kufanya kazi mechi tatu za kwanza japo Chelsea alikuwa akipata ushindi mwembamba huku mipango ya upataji goli ilikuwa ni shida, lakini pia si tu kwenye ushambuliaji bali hata kwenye safu ya ulinzi kwani Chelsea ilikuwa ikipata shida. Na ndipo hapo mashabiki wa Chelsea walianza kumlilia Conte amuanzishe Fabregas kutokana na kwamba timu ilikuwa ikikosa ufundi hususani kwenye kiungo na ushambuliaji

Gundu lilianza kwenye mchezo dhidi ya Swansea ambapo Chelsea walipata sare ya 2-2, Cahill akifanya madudu huku mechi mbili zilizofuata dhidi ya Liverpool na Arsenal ndio hali ikawa mbaya zaidi kitu ambacho kilinisukuma kuandika niliyoyaandika.

cahill

Gary Cahill (byeusi) akifanya makosa yaliyomfanya Leroy Ferwa Swansea (nyeupe) kuupata mpira na kwenda kufunga bao

Kipigo cha Arsenal kilimfungua Conte akili kwani kwa muda mrefu alikuwa akihangaika na mfumo wa 4-1-4-1 ambao haukuwa na msaada tena na sasa akaamua kucheza karata yake ya mwisho ambayo sioni shida kuiita kama kamari ya kutumia mfumo wa 3-4-3.

Sote tunajua kuwa Conte ni muumini mkubwa wa mfumo wa 3-4-3, lakini alichokuwa anakifanya mwanzoni mwa msimu ni kutafuta uwiano wa wachezaji ili aweze kuutumia mfumo huo kitu ambacho naweza kusema kilimgharimu (Subira yavuta heri lakini kwa hapa ilishindikana) na baada ya kipigo cha Arsenal, ndipo Conte uzalendo ulimshinda na kuamua kutoa makucha yake na kujaribu bahati yake katika hilo. Na hapo ndipo 3-4-3 ikaanza.

Kwenye mfumo huu mpya wa 3-4-3 tumepata kuona maingizo mapya kama vile Victor Moses ambaye awali nilihisi kama asipotolewa tena kwa mkopo basi atasugua sana benchi  na pia tukauona usajili mpya, Marcos Alonso ambapo wawili hao wanachezeshwa kama mawinga wakabaji huku Cesar Azpiliqueta akibadilishiwa majukumu kutoka beki wa kushoto hadi kuwa beki wa kati sambamba na Gary Cahill na David Luiz ambaye alichukua nafasi ya Terry aliyepata majeruhi kwenye mchezo dhidi ya Swansea.

Kwa mfumo huo pia tunaona viungo N”Golo Kante na Nemanja Matic wakiungana na Victor Moses na Marcos Alonso kutengeneza safu ya kiungo ya watu wanne huku mbele yao kukiwa na washambuliaji watatu ambao ni Eden Hazard, Willian/ Pedro na Diego Costa.

Mechi ya kwanza mfumo huu kutumika dhidi ya Hull City Chelsea walichomoza na ushindi wa mabao 2-0, akafata Leicester City akapigwa 3-0, Manchester United 4-0, Southampton 2-0 na kisha leo hii Everton akila 5-0 watoto wa uswahili wanasema “Mkono”

MFUMO HUU UMEIBADILISHAJE CHELSEA?

Kuwepo kwa Moses na Marcos Alonso ambao wanacheza kama mawinga wakabaji ndipo Conte alipofanya heko. Kama ingekuwa ni kwenye mchezo wa karata aina ya Arubastini basi tungesema Conte amelamba dume.

Victor Moses na Marcos Alonso wakishangilia moja ya mabao

Victor Moses na Marcos Alonso wakishangilia moja ya mabao

Moses na Alonso ni wachezaji ambao wamekuwa wakileta uwiano (balance) kwenye kikosi cha Chelsea kuanzia nyuma hadi mbele kitu ambacho kinawafanya Chelsea kukaba na kushambulia wakiwa na idadi sawa ya wachezaji. Hiki ndicho kitu ambacho Chelsea ilikuwa ikikikosa kwenye mfumo wa 4-1-4-1.

KWENYE UKABAJI

Mpira ukiwa kwa adui, Chelsea inakaba ikiwa na watu saba ambao ni mabeki watatu wa kati (Azpiliqueta, Cahill, Luiz), viungo wawili wa kati ambao ni Kante na Matic pamoja na mawinga wakabaji ambao ni Alonso na Moses. Wakikaba wachezaji saba nyuma ni vigumu kupenya ngome yao hiyo ambapo Cahill na Alonso wanazuia mashambulizi kutoka kushoto, Azpiliqueta na Moses wanazuia mashambulizi kutoka kulia huku Luiz akisaidiana na Kante na Matic kuzuia mashambulizi kutokea katikati na ndio maana sishangai Chelsea kucheza mechi tano mfululizo kwenye EPL bila kuruhusu bao.

ngolo

N’Golo Kante

KWENYE KUSHAMBULIA

Chelsea ikiwa inashambulia lango la adui inakuwa na watu saba mbele ambao ni pamoja na washambuliaji watatu (Costa, Willian/Pedro na Hazard), mawinga wakabaji (Moses na Alonso) ambao hugeuka mawinga washambuliaji pamoja na viungo wa kati ambao ni Kante na Matic ambapo hushambulia kutokea kati kati ya uwanja na ndio maana sishangai kuona Chelsea ikifanikiwa kufunga magoli 16 kwenye mechi tano za EPL

Eden Hazard akishangilia moja ya mabao aliyofunga msimu huu

Eden Hazard akishangilia moja ya mabao aliyofunga msimu huu

Kwa kifupi ni kuwa Chelsea inashambulia ikiwa na watu saba mbele na inazuia ikiwa na watu saba nyuma na huo ndio uwiano nnaouzungumzia na hata ikitokea wakapokonya mpira kwa adui, bado wana uwezo wa kushambulia kwa kushtukiza (Counter attack) kwani wana uhakika wa watu watatu mbele ambao ni Pedro, Costa na Hazard ambao hukaa karibu na mstari wa kati kusubiria mipira iliyonyang’anywa.

Na ndio maana kwenye mechi ya usiku wa leo licha ya Everton kuanza na mabeki watano nyuma lakini walishindwa kuhimili vishindo vya washambuliaji saba wa Chelsea

UMUHIMU WA MFUMO HUU:

  1. Chelsea inacheza ikiwa na idadi sawa ya wachezaji kwenye kukaba na kushambulia huku shukrani za pekee ziwaendee Moses na Alonso ambao wanakaba na kushambulia kwa wakati mmoja kutokea pembeni. Chelsea ikishambulia wanakuwa mawinga washambuliaji na Chelsea ikikaba wanageuka kuwa mawinga wakabaji.Tatizo la uwiano wa timu limesuluhishwa kwa staili hii.
  2. Washambuliaji watatu wanaocheza nafasi ya ushambuliaji wanapata uhuru wa kushambulia kwani wanalindwa vyema na wenzao waliopo nyuma na pembeni hivyo hawana haja ya kurudi nyuma kusaidia kukaba. Hii ndio sababu pekee inayomfanya Hazard kurudi kwenye kiwango chake maana anacheza kama mchezaji huru uwanjani na ndio maana ameweza kufunga magoli matano kwenye mechi nne za mwisho hal kadhalika Costa ambaye anafunga karibia kila mechi kwa sasa. Tatizo la Hazard kucheza chini ya kiwango limetibiwa kwani kwasasa anachowaza uwanjani ni kushambulia tu na ndio tunapata kuona kiwango chake halisi.
  3. Safu ya kiungo imeimarika tofauti na hapo awali kwani inapata msaada mkubwa kutokea pembeni kwa Moses na Alonso na kutokea nyuma kwa Luiz, Cahill na Azpiliqueta. Hakuna jinsi ambayo unaweza kusema kiungo kinapwaya kwa sasa na ndio maana katika michezo hiyo mitano mfululizo, Chelsea amekuwa akiongoza kwa umiliki wa mpira na upigaji pasi.
  4. Kujiamini kwa timu kumeongezeka maana kila idara inasaidiana na idara nyingine kuhakikisha matokeo yanapatikana, idara ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji zina mahusiano mazuri hali inayomfanya Luiz kutulia na kucheza kwa kufuata mlolongo maalum wa pasi, hali inayomfanya Cahill kutulia na kuacha papara kwani anacheza akiwa amezungukwa na wachezaji wenzake huku pia Courtois akitoa maelekezo na kulinda vyema lango lake akiwa amezungukwa na timu nzima.

Kwasasa sisikii kelele za mashabiki wa Chelsea wakimlilia Fabregas kwenye idara ya upishi wa magoli kwani kwa sasa Chelsea haitegemei mtu mmoja kutengeneza nafasi. Hazard na Pedro wanafunga lakini pia wanamlisha Costa vyema. Matic na Kante wanapiga pasi mbele kwa wakati huku pia Moses na Alonso wakipiga krosi safi na kufunga pia.

Kwa kifupi ni kuwa Conte alifanya jambo sahihi la kuhamia kwenye mfumo wake wa kidigitali (3-4-3) kwani ile analogia aliyokuwa akiijaribu (4-1-4-1) ilikuwa ikimpotezea muda.

Gari limewaka…….!!!!!!!

 

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets