Menu

MWILI WA GEORGE LWANDAMINA, AKILI ZA ANTONIO CONTE; HII NDIYO YANGA MPYA NDANI YA MFUMO WA 3-4-3.

Na Adam Mbwana,

Bila shaka utaikumbuka Bayern Munich iliyotwaa Ubingwa wa UEFA mwaka 2001 ikiwa chini ya kocha Mjerumani Ottmar Hitzfeld wakitumia mfumo wa 3-4-3 wa mabeki watatu nyuma ambao ni Linkem, Andersson na Kuffor, wakitumia mawinga wawili wakabaji ambao ni Lizarazu na Sagnol na viungo wawili wa kati ambao ni Effenberg na Hagreaves huku wakiwa na washambuliaji watatu mbele ambao Salihamidzic, Scholl na Elber wakimtandika Valencia kwenye mchezo wa fainali kwa mikwaju ya penati.

Bila shaka utaikumbuka Korea Kusini iliyokuwa mwenyeji wa Kombe la dunia mwaka 2002 ikiwa chini ya mholanzi, Guus Hiddink ilivyoutumia mfumo huu wa 3-4-3 bila kuisahau Barcelona ya Kocha Johan Cruyff kuanzia miaka ya 1988 ikifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali

Lakini pia utamkumbuka Kocha Marcelo Biesa tangu akiifundisha klabu ya Newell Old Boys ya nchini Argentina miaka ya 1990 na baadae timu ya taifa ya Argentina kuanzia mwaka 1998 na timu ya taifa ya Chile ya mwaka 2010 kwenye kombe la dunia na mpaka sasa akiwa na klabu ya Lazio ya nchini Italia. Kwa muda wote huo Biesa amekuwa ni muumini mkubwa wa mfumo huu.

Tusiende mbali sana, bali tumuangazie Antonio Conte ambaye tangu akiwa Juventus amekuwa akitumia mfumo huu, akaenda timu ya taifa ya Italy na mwaka huu kwenye michuano ya Euro tuliona alivyokuwa moto wa kuotea mbali na hadi sasa akiwa na Chelsea akicheza michezo mitano bila kuruhusu goli hata moja.

Tuachane kwanza na Conte na wenzake, turudi kwenye mada yetu ya leo halafu taratibu tutaanza kuelewa maana ya mifano hiyo.

Hatimaye ndoa ya kocha Mholanzi Hans Van der Pluijm na Yanga imevunjika baada ya kudumu kwa mafanikio makubwa huku Mholanzi huyo akikumbukwa kwa umahiri wake wa kutumia mifumo ya 4-4-2 na 4-3-3 muda mwingine kupata matokeo. Lakini ujio wa kocha mpya, George Lwandamina kutoka Zesco United ya Zambia ni wazi kuwa kocha huyo atakuja na mbinu nyingine mpya za kifundi ambazo huenda zitatufanya tuishuhudie Yanga ikitumia mfumo mpya wa kiuchezaji aidha kwa kutumia wachezaji wale wale au kuongeza baadhi wapya ili kuendana na matakwa ya mfumo wa kocha na falsafa zake.

 

Ebu tufanye Bongo Movie kidogo;

Najaribu kuvaa viatu vya kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina japo kwa jina tu halafu natumia fikra zangu binafsi ambazo bila shaka hazipo kwenye fikra za Lwandamina. Najaribu kujipa majukumu ya ukocha kwenye kikosi cha Yanga kwa kutumia mfumo wa 3-4-3 ambao hatujazoea kuuona aghalabu hapa kwetu Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Najaribu kutumia kikosi kilekile cha Yanga kilichopo na kukiingiza kwenye mfumo huu nione kama kitaweza kufit ingawa nahisi wengi watashangazwa na mabadiliko haya ya ghafla.

Picha linaanza Yanga ikitumia mfumo wa 3-4-3 ambapo nyuma kunakuwa na walinzi watatu, katikati viungo wanne na washambuliaji watatu.

kikosi

 

SAFU YA ULINZI:

Katika mfumo huu na kwa kikosi cha sasa cha Yanga kilivyo, walinzi watatu wa nyuma ni VINCENT BOSSOU, KELVIN YONDANI na VINCENT ANDREW ‘DANTE’

Mfumo huu unahitaji walinzi watatu wenye sifa ya urefu, wenye nguvu na wazuri kwenye mipira ya juu ambao wana mawasiliano mazuri na pia kila mlinzi kati yao anajua kukabana na mshambuliaji katika hali ya mmoja kwa mmoja (man to man situation).

Kigezo cha kumchagua Yondani, Bossou na Dante ni kwamba watatu hawa wamekuwa wana mawasiliano mazuri na wanaelewana kwani mara kwa mara kocha Hans van der Pluijm amekuwa akiwachezesha wawili wawili mara kwa mara. Kama sio Bossou na Dante, basi ni Bossou na Yondani au Yondani na Dante na kila mara wanapocheza pamoja basi safu ya ulinzi ya Yanga inakuwa imara.

Kwa kigezo cha urefu wa mabeki hao, ni Bossou tu ndiye atakayefaulu kwani si Yondani wala Dante ambao wanaweza kukabana na washambuliaji wenye miili mikubwa na wajanja wajanja kama wale wa timu za Afrika Magharibi au Kaskazini hususani katika mipira ya juu ambayo huwahitaji kuruka juu zaidi kuicheza kabla ya mshambuliaji, hivyo ni wazi kuwa kwa kigezo hiki, bila shaka ningeihitaji kusajili beki mwingine wa kati wa aina ya Bossou kwa maana ya urefu na umbo kubwa pia. Sina maana kwamba Dante na Yondani hawafai, lakini kwa michuano ya kimataifa bila shaka Bossou mwingine angehitajika ili kuweka uimara wa safu ya ulinzi.

 

SAFU YA KIUNGO

Kwa mfumo huu mpya, bila shaka mashabiki wa soka wangetegemea kuona kitu kipya kutoka kwangu kwani bila shaka wengi mmeshajiuliza nafasi ya mchezaji bora wa VPL msimu uliopita, Juma Abdul huku wengine mapovu yalishaanza kuwatoka mkidhani nimemuuza Simba au Azam. Lahasha! Juma Abdul ana kazi mpya kubwa zaidi.

Kwenye safu ya kiungo, wachezaji wanne wangehusika, wawili wa pembeni na wawili wa kati. Viungo hawa wa pembeni bila shaka kwenye kikosi change ungewakuta HASSAN KESSY na JUMA ABDUL ambao kwa jina la kitaalam ungeweza kuwaita Mawinga wakabaji (Wing Backs) ambao kazi yao kubwa ingekuwa ni kupanda na kushuka. Watu hawa wawili katika hali ya kawaida wanatakiwa wawe ni watu wenye mapafu ya mbwa ambao hawachoki wenye uwezo wa kupandisha mashambulizi wakati timu ikiwa na mpira na kurudi nyuma kwa kasi kukaba wakati timu ikiwa haina mpira.

Katika ushambuliaji, wawili hawa wanatakiwa kwanza wawe wanajua kupiga krosi zilizoshiba, na bila shaka tunaujua uwezo wa Juma Abdul na Hassan Kessy katika hizo kazi. Wawili hawa wanaweza kupandisha timu kwa kasi na kupiga krosi murua kwa washambuliaji kufunga ndani ya boksi au wakaingia wenyewe na kupiga pasi aina ya V au hata kupiga mashuti wao wenyewe golini kama mawinga huku pia wakiweza kurudi nyuma kukaba kama mabeki wa pembeni, nafasi ambayo ndio wameizoa kucheza. Katika kikosi cha Yanga cha sasa ni Abdul na Kessy ndio wenye sifa hizo kwani ni wepesi, wana kasi, na wanaweza kurudi kwa haraka kusaidia timu kukaba.

wingers

Majukumu ya viungo wa pembeni wa Yanga ya kukaba na kushambulia uwanjani ili kuleta uwiano wa timu

Hawa ndio wachezaji muhimu kwenye kikosi chote kwani ndio wanaoleta uwiano mzuri kwenye ushambuliaji na ukabaji kutokana na kwamba hufanya kazi zote hizo kwa wakati mmoja na kuwafanya mabeki watatu wa kati kulindwa kutokea pembeni halikadhalika kuwafanya washambuliaji wangu watatu kusaidiwa kuletewa mipira kutokea pembeni wakati wa kushambuliaji.

Wachezaji wengine wanaoweza kucheza katika nafasi hii kama Juma Abdul na Kessy hawatakuwepo ni Juma Mahadhi, Deus Kaseke, Oscar Joshua, Haji mwinyi na Mbuyu Twite japo sio kwa kiwango kikubwa kama ambavyo Kessy na Abdul wangecheza.

Ukiachana na viungo hao wa pembeni, lakini pia kuna viungo wawili wa katikati ambao katika mfumo wangu huu mpya itachukuliwa na HARUNA NIYONZIMA na THABAN KAMUSOKO. Kwa kifupi ni kuwa, Viungo wawili wanaocheza kwenye nafasi hii mmoja huwa na sifa ya kiukabaji ambapo husaidiana na mabeki watatu wa nyuma na mwingine huwa na sifa ya kiushambuliaji zaidi ambapo husaidiana na washambuliaji watatu wa mbele kikamilifu.

kuzu

Viungo wa Yanga watakavyokuwa wakiungana na walinzi wa timu hiyo kukaba endapo timu pinzani ikiwa na mpira

Nafasi ya kiungo wa kati mkabaji ambaye angesaidiana na mabeki watatu inakwenda kwa Kamusoko ambaye mara nyingi huwa tunamuona akirudi nyuma kusaidiana na mabeki na kuanzisha mashambulizi kupitia pembeni au kupanda nayo na kuileta mbele moja kwa moja kwa washambuliaji. Kamusoko ni mzuri katika kutuliza kiungo na ana umbo kubwa na zuri linalomuwezesha kutibua mipango ya adui japokuwa si mwepesi sana hususani katika kufanya (tackling) kitu ambacho kingenilzimu kuingia sokoni kutafuta kiungo wa aina hiyo ambaye ni mwepesi, mwenye kasi na mzuri katika kutibua mipango ya adui. Bila shaka taarifa za uji wa kiungo MESHACK CHAILA kutoka Zesco zingekuwa njema sana kwangu kwani najua angeweza kufanya kazi hiyo vyema. Kwa hapa nasikitika kusema kuwa Kamusoko angeanzia benchi ingawa si mara kwa mara.

Nafasi ya kiungo wa kati wa ushambuliaji ingekwenda kwa Haruna Niyonzima ambaye sisi wote tunamjua kwa ufundi wa kupiga pasi mshororo, kushambulia kwa kasi na kurahisisha kazi ya washambuliaji waliopo mbele yake. Kazi kubwa ya Haruna ingekuwa ni kupandisha timu mbele na yeye ndiye angekuwa injini kubwa katika usakaji wa magoli. Nafasi hii pia Kamusoko anaweza kucheza endapo kama nikimpata Chaila lutoka Zesco kwani Kamusoko na Haruna wana vitabia vinavyofanana fanana hivyo ningefurahi kuona mpambano kati yao wa kugombea namba. Ila kwa sasa waache waanze wote tuone.

kusha

Viungo wa Yanga watakavyokuwa wakiungana na washambuliaji wa timu hiyo katika mashambulizi pindi watakapokuwa wakiumiliki mpira

Kwa kifupi katika safu yangu ya Kiungo yupo Hassan Kessy, Juma Abdul, Thaban Kamusoko na Mbuyu Twite. Lakini pia Juma Makapu na Mbuyu Twite wanaweza kucheza kwenye nafasi hiyo. Hii ni nafasi ambayo muhimu sana uwanjani ambayo inahusika pande zote mbili na kukaba na kushambulia na inahitaji maelewano makubwa katika kupishana kwani ndiyo inayounganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji. Mawasiliano na Maelewano ndiyo nguzo yao kuu.

 

SAFU YA USHAMBULIAJI:

Kwenye safu yangu ya ushambuliaji, bila shaka ungewakuta watu watatu ambao ni DONALD NGOMA, SIMON MSUVA na AMISSI TAMBWE.

Msuva ndiye angekuwa mchezaji huru kwenye kikosi changu kwani uwezo wake wa kukimbia kwa kasi na kuwatoka mabeki kingekuwa ni msaada mkubwa katika mambo mawili. Kwanza atakuwa msaada mkubwa kwa washambuliaji wenzake wawili ambapo mara nyingi atakapokuwa anakimbia na mpira kuelekea kwenye boksi bila shaka mabeki wa timu pinzani watakuwa wakimuangalia yeye tu wakati huo Amissi Tambwe na Ngoma wanafungua nafasi kitu ambacho kinampa maamuzi matatu, Moja ni kutoa pasi kwa mmoja kati ya washambuliaji wawili ambao watakuwa peke yako katika nafasi za kufunga, Mbili ni aingie mwenyewe kwenye boksi apige endapo kama mabeki watamuacha na kuwafuata kina Tambwe au tatu atoe pasi kwenye winga ambazo wamefungua Kessy na Abdul halafu aungane na Tambwe na Ngoma kusubiri krosi ndani ya boksi.

Majukumu ya Simon Msuva katika nafasi yake ya ushambuliaji akiwa mbela ya viungo wanne na nyuma ya washambuliaji wawili

Uzuri wa Msuva ni kwamba anaweza kufunga na ndio maana sishindwi kusema kuwa anaweza kufunga karibia kila mechi kutokana na ukweli kwamba endapo akicheza kama mchezaji huru uwanjani katika eneo la nyuma ya washambuliaji, anaweza kufunga mwenyewe au kutoa pasi za magoli. Kwanini asiwe mchezaji bora wa msimu?

Nafasi hii ya Msuva pia inaweza kuchukuliwa na Deus Kaseke au Obrey Chirwa. Hivyo Msuva hatatakiwa kubweteka sana kwani wapinzani wake hao wa namba wanaweza kufit vyema kwenye mfumo huu pia.

Endapo kama Ngoma, Tambwe na Msuva wakielewana vyema na wakiju maeneo yao ya kukimbilia basi bila shaka watakuwa ni moto wa kuotea mbali

 

KWA UJUMLA:

Kwa mfumo huu, Yanga itaweza kushambulia ikiwa na wachezaji saba na kukaba ikiwa na wachezaji saba kitu ambacho kitaleta uwiano mzuri wa timu na mawasiliano yatakuwa ni rahisi sana miongoni.

Kwenye kushambulia, Yanga itakuwa na wachezaji saba ambao ni Tambwe, Ngoma, Msuva (Kutokea mbele), Niyonzima na Kamusoko (Kutokea katikati) na Kessy na Juma Abdul (Kutokea pembeni)

Kwenye kukaba, Yanga itakuwa na wachezaji saba pia ambao ni Bossou, Yondani na Dante (Kutokea nyuma), Kamusoko na Niyonzima (Kutokea katikati) na Kessy na Juma Abdul (kutokea pembeni)

Matakwa makubwa ya mfumo huu ni MAELEWANO na MAWASILIANO baina ya wachezaji uwanjani. Wachezaji inabidi wapate muda mrefu wa kufanya mazoezi kwa pamoja ili wazoeane na mimi kama kocha ningehitaji uongozi wa Yanga ufanye usajili wa beki wa kati na kiungo mkabaji haraka iwezekanavyo ili niweze kuanza maandalizi mapema ya kuleta muunganiko wa timu kupitia kauli mbiu kuu mbili za Maelewano na Mawasiliano. Bila shaka ningekuwa mkali kwa wachezaji wakati wa  mazoezi kwani nisingependa uzembe wa aina yoyote ile na ningependa wachezaji wangu wajitolee kucheza kwa moyo wawapo uwanjani.

Usishangae kuona sijataja Golikipa, kwani bila shaka DEOGRATIUS MUNISHI ‘DIDA’ ngekuwa chaguo langu la kwanza kutokana na uwezo wake wa kuusoma mchezo na kupanga vyema safu yake ya ulinzi huku akisaidiwa vyema na umbo lake refu ambapo sitakuwa na wasiwasi sana kwenye mipira ya kona wakati wa kushambuliwa

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets