Menu

KARIBU LWANDAMINA: UTAIFUNDISHA YANGA LAKINI MWAJIRI WAKO NI SIMBA.

Na Adam Mbwana,

Hayawi hayawi sasa yamekuwa!, walosema hasaini sasa kasaini!

Hivi ndivyo nnavyoweza kuimba kwa sasa hasa baada ya Yanga kumtangaza rasmi Lwandamina kuwa kocha wao mpya leo, zoezi lililotanguliwa na kusaini mkataba wa miaka miwili huku akichukua nafasi ya Pluijm ambaye atakuwa Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo.

Hatimaye yamekuwa na sasa sio tetesi tena…Sipo karibu na mitaa ya Twiga na Jangwani kunako viunga vya Kariakoo lakini nazisikia kelele za ngamia wakisindika nyayo zao ardhini na kupeperusha mikono juu wakiimba ule wimbo maarufu ambao unawakera sana wale ndugu zangu wa rangi ya bluu na nyekundu “waacheni waandamane ieeeeee…..wajinga waleee….mkodisho mbele mbele kwa mbele….” Hahaha….!!! natania tu jamani wala “msi-kechi filings”. Huwezi kuamini nipo Tegeta lakini kelele hizo nazikia.

Huku upande wa pili kwa wale wanaoitwa wa Matopeni…dah..!! samahanini jamani sijui kwanini leo naropoka sana anyway…Nao wapo kwenye jengo lao kule juu kabisa mitaa ya Msimbazi wakichungulia madirishani jinsi Ngamia wanavyomuingiza mwali wao ndani. Wameshamaliza kula nyama zao wapo na vijiti mdomoni wakichokonoa meno huku wengine wakisema “Huyo Lwandamina hana muda mrefu anasepa…” wengine wakageuka watabiri eti wakidai kuwa Mzambia wa watu hachukui hata mwezi……………Nyie acheni roho mbaya.

Nijuavyo mimi Lwandamina ni kocha bora maana kwa mafanikio yake akiwa na Zesco mpaka kuifikisha timu hiyo hatua ya nusu fainali ya Klabu bingwa barani Afrika sio kitu cha mchezo tena nakikumbuka kile kipigo kitakatifu cha mabao 3-1 alichomshushia bwana Zamaleck pale uwanja wa Ndola. Ubora wa kocha huyu ni mkubwa hususani katika michuano ya kimataifa kwani wote tumeshuhudia kuwa hata hatua hiyo ya nusu fainali aliyoishia ni kwamba alitolewa na bingwa mtetezi Mamelod Sundown ….

Nisiongee mengi ila nipende tu kumkaribisha Bwana Lwandamina na hivi asubuhi tu nimetoka kumsoma magazetini akidai kuwa atakuwa mkali sana kwa wachezaji wazembe, na huyu bwana hatanii maana nasikia alishawahi kumtwanga vibao shabiki enzi zake akiwa Zesco. Sijui kweli…..!!!

Nimkaribishe Lwandamina kwa kumueleza ukweli, hata kama nyinyi mmeamua kumficha. Huku Tanzania sio kama Uingereza, Ufaransa, Hispania au hata Italia au tusiende mbali, huku Tanzania sio kama kule Zambia alipotoka. Huku kwetu Tanzania ligi yetu ina timu 16 kinadharia, lakini kivitendo ligi yetu ina timu mbili tu na ndio maana nikasikia juzi Manara anasema simba ipo radhi kutoa hata Milioni 20 kuleta refa kutoka nje kuchezesha mechi ya Simba na Yanga ya mzunguko wa pili ambayo yeye Lwandamina atakuwa akiliongoza benchi la ufundi kama akijaliwa uzima. Bila shaka utaona jinsi mechi hiyo inavyochukuliwa kwa uzito mkubwa.

Hakuna ubishi kwamba yeye sasa ni kocha wa Yanga, lakini akubali ukweli kuwa meneja wake ni Simba kwani atakapochanga karata zake vibaya kwenye mechi yake dhidi ya Simba basi ajue amelikoroga, na waswahili wanasema ukilikoroga utalinywa, au mchuma janga hula na wa kwao, sasa hili atalila mwenyewe.

Kwani uongo…? au mpaka tuanze kutaja orodha ya mameneja wa Yanga waliofukuzwa kazi kutokana na kufungwa na Simba? Siwezi kupoteza muda katika hilo kwani si mnamkumbuka yule aliyefukuzwa kazi siku chache baada ya kufungwa kwenye mechi ya Mtani jembe? sasa kwanini nisumbuke wakati mnawajua. Huyo Pluijm mwenyewe mambo yameanza kumuendea kombo baada ya kutoa sare ya 1-1 mechi dhidi ya Simba raundi ya kwanza…wenye timu wakidai kuwa oooh timu ilicheza vibaya tena hao “wenye timu” wakijidai kusema eti “Tumecheza na Simba pungufu na bado tumetoa sare na tumezidiwa kipindi cha pili, sasa kama wangetimia si tungefungwa kabisa? Huyo kocha hafai aondoke tu….”  

Mhhh…!!Maisha ya Simba na Yanga ni ya kusadikika. Ukifungwa na Kagera Sugar watakuelewa lakini sio ufungwe na Simba au Simba afungwe na Yanga.

Lwandamina lazima ajue kuwa anakutana na mashabiki wenye mihemko ya hali ya juu..mashabiki ambao dakika mbili nyingi wanakugeuka. Uzuri ni kwamba yupo karibu na mhanga wa mihemko ya mashabiki (Pluijm) kwahiyo atamsimulia vizuri kilichotokea.

Karibu lwandamina, Simba ana uwezo wa kukufanya upendwe na mashabiki na viongozi wa Yanga au ufukuzwe kazi……Kama huamini kamuulize Mzambia mwenzio, Patrick Phiri akwambie kwanini mpaka leo mashabiki wa Simba wanamhusudu.

Karibu Bongoland uling’ong’ose fupa lililomshinda fisi.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets