Menu

KIFO CHA MCHEZAJI ISMAIL KHALFAN KIMETUKUMBUSHA SUALA LA MSINGI SANA KWENYE SOKA LETU

Na Adam Mbwana,

Wakati dunia ya wapenda soka bado ikiwa kwenye majonzi na maombolezo ya vifo vya wachezaji na wataalamu wa benchi la ufundi wa klabu ya Chapecoense ya nchini Brazil baada ya kupata ajali ya ndege wakiwa njiani kuelekea nchini Colombia kwenye mchezo wa fainali ya kombe la Sudanamericana usiku wa kuamkia Novemba 29, mengine mazito na ya kusikitisha yameshajitokeza tena hapo jana hapa kwetu nchini.

Huko kunako dimba la Kaitaba mjini Bukoba ambapo kuna mechi za ligi ya vijana wa U-20, kumejitokeza msiba mzito wa mchezaji Ismail Khalfan wa Mbao FC wakati timu yake ikiwa dimbani kuvaana na vijana wenzao wa Mwadui FC.

Ni habari ambazo zinasikitisha na kuleta simanzi kubwa kwenye tasnia ya soka na michezo kwa ujumla hasa baada ya picha na video mbalimbali kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha jinsi kijana huyo mwenyeji wa Mwanza alivyokumbwa na mauti wakati timu yake ikiwa mbele kwa bao moja alilolifunga yeye kwa kisigino mnamo dakika ya 29 ya mchezo huo.

Lengo langu sio kuelezea yaliyojiri mpaka kijana wetu Ismail kufikwa na mauti hayo kwani naamini kuwa kila mtu kama sio kusikia habari hii basi ameona picha au kutazama video hiyo, huku shukrani za pekee zikiieendea Mitandao ya kijamii ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kufikisha taarifa kwa umma kwa muda muafaka.

Moja ya mambo ambayo yamenisukuma kuandika makala haya na ambayo sina budi kusema ukweli kuwa yalinishangaza kwenye tukio hilo ni pamoja na kutokuwepo kwa gari la kusafirishia wagonjwa maarufu kama “Ambulance” kwenye uwanja huo wa Kaitaba, hali ambayo ilipelekea marehemu kupelekwa hospitali ya mkoa kwa kutumia gari la zima moto na ndipo hapo nikaanza kujiuliza maswali kadhaa ambayo sikupata majibu.

Je, ni kawaida kwa Uwanja wa Kaitaba kutokuwa na Ambulance wakati mechi zikiendelea?, Je ni kwa mechi hizi tu za U-20 ambapo kunakuwa hakuna Ambulance au hadi zile za Ligi ya wakubwa? Nini haswa kilitokea?

Naomba nieleweke kwamba sina nia ya kuutupia lawama upande wowote kutokana na kifo hiki kwani naamini katika hali ya ubinadamu kila mtu ana majonzi juu ya kifo hiki kilichotokea ghafla. Si wachezaji wa timu zote mbili, viongozi wa timu hizo, makocha na jopo la ufundi, Viongozi wa soka nchini, watu wa huduma ya kwanza, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Ismail na wapenda soka wote kwa ujumla ndani na nje ya mipaka ya nchi hii wote tumesikitishwa na tukio hili na bado tuna uchungu, lakini uchungu wetu usitufanye tushindwe kuhoji mambo ya msingi ambayo pengine yataweza kuzuia tatizo mbele ya safari kwasababu maisha bado yanaendelea.

Hakuna taarifa inayosema kuwa mauti yalimkuta marehemu Ismail kwasababu ya kucheleweshwa hospitalini kwani gari la zima moto liliweza kufanya jitihada kubwa japo sio kazi yake na ndio maana tunaamini kuwa haya ni mapenzi ya Mungu kwa kijana wetu kutangulia mbele za haki. Huwezi kujua kwani huenda hata Ambulance ingekuwepo uwanjani kama yalikuwa ni mapenzi ya Mungu bado isingeweza kuokoa maisha ya kijana wetu kama ilivyokuwa miaka 13 iliyopita kwenye kifo cha nguli wa soka wa Cameroon, Marc-Vivien Foe ambaye alifariki papo hapo huko nchini Ufaransa licha ya kuwepo kwa kila kitu ambacho kingeweza kuokoa uhai wake kuanzia jopo la madaktari mahiri wa wachezaji, Ambulance na vingine vingi. Lakini hayo yote hayatufanyi tushindwe kuhoji umuhimu wa kuwepo kwa Ambulance viwanjani ambapo muda wowote mchezaji anaweza kuumia.

khalfan

Taarifa za uhakika kabisa kutoka kwa wenyeji wa mkoa wa Kagera ambao mara kwa mara wamekuwa wakishuhudia mechi hizo za U-20 tangu zilipoanza, zinadai kuwa hakujawahi kuwa na Ambulance kwenye mchezo wowote ule unaofanyika uwanjani hapo lakini kwenye zile mechi za ligi ya wakubwa yaani (Ligi Kuu Soka Tanzania Bara) Ambulance huwa zinakuwepo.

Hili ndio jambo linaloniongezea huzuni kabisa na kunifanya nijiulize mara mbili mbili kwanini mechi za Ligi Kuu kuwepo na ambulance lakini sio ligi hizi za vijana? Je, hawa vijana hawana haki hiyo ya msingi kwa ajili ya usalama wa afya zao?

Wakati tunaomboleza msiba huu mzito wa kijana wetu Ismail Khalfan, sisi kama viongozi wa timu, wachezaji, viongozi wa vyama vya soka, wataalamu wa mabenchi ya ufundi na mashabiki tutafakari pia umuhimu wa afya za vijana wetu ambao wanacheza na kutufanya tufurahie soka.

Wewe kama kiongozi wa timu hakikisha uwanja unaopeleka timu yako kucheza una kila hitaji muhimu, usihangaikie tu usafiri wa kukufanya uwahi uwanjani kwa wakati, bali pia uangalie vitu vya msingi kama Ambulance ambavyo vinaweza visionekane kuwa na umuhimu lakini kumbe ni vya msingi sana. Wewe kama msimamizi wa mechi unapokuwa unakagua timu kama zimefika uwanjani kwa wakati basi pia usisahau kukagua kama kila kitu kinachowezesha kulinda afya za wachezaji kipo sawa na wewe kama meneja wa uwanja usiishie tu kukagua miundombinu ya uwanja kama ipo salama kabla na baada ya mchezo, bali pia hakikisha kila nyenzo inayohusika na usalama wa afya za wachezaji ipo mahala pake.

Sisi kama familia ya soka tuungane katika kukumbushana masuala ya msingi kama haya na si kuishia kuangalia mapato ya mechi na matokeo ya uwanjani kwani Soka ni zaidi ya hapo na kila mtu atimize majukumu yake na sio kufanya mambo hobela hobela. Soka ni mchezo mzuri kwa mtazamaji na mchezaji lakini pia ni hatari sana kama hakutakuwa na uhakika wa usalama wa afya za wachezaji. Na ndio maana kuna madaktari wa timu na watu wa huduma ya kwanza ambao wanaajiriwa na kulipwa mishahara mikubwa kwasababu ya kazi hizo. Wakati unakumbuka kuwapigia simu watu wa zima moto walete gari uwanjani, pia kumbuka kuwapigia watu wa Ambulance wafanye hivyo.

Napenda kuwapa pole familia ya Marehemu kijana wetu, Ismail Khalfan ambaye huenda miaka ya baadaye angekuwa ni tunu kubwa kwa taifa. Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu cha simanzi na masikitiko. Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe. Pumzika kwa amani Ismail.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets