Menu

SIMBA NA YANGA ZINAPONZWA NA HISIA; LWANDAMINA NA OMOG WAWE MAKINI SANA

Na Adam Mbwana, 

Weekend ilikuwa ndefu bila shaka kwa baadhi ya watu lakini sio kwa mashabiki wa soka ambao walikuwa ‘busy’ kuendelea kuzifuatilia timu zao. Baada ya Ligi Kuu Soka Tanzania bara kusimama, mashabiki wamekuwa makini sana kufuatilia habari za usajili kwa timu zao hususani kwa mashabiki wa Simba na Yanga ambao wamekuwa wakitambiana kwa maneno ya hapa na pale kuhusiana na wachezaji wao wapya wa kigeni

Baada ya sajili za hapa na pale, sasa ulifika muda wa vilabu hivi vikongwe hapa nchini kucheza mechi za majaribio ili makocha Joseph Omog kwa Simba na George Lwandamina kwa Yanga kuwapima wachezaji wao wapya na mwenendo wa timu zao kwa ujumla. Shughuli ikaanzia hapo….!!!!

Simba ilitupa karata yake ya kwanza ya kirafiki dhidi ya Polisi Moro siku ya sherehe za Uhuru tarehe 9 na kufanikiwa kushinda kwa mabao 2-0 ya Abdi Banda na Ibrahim Ajib na hali ikawa shwari. Siku iliyofuata ya Jumamosi jirani zao Yanga wakachezea kichapo cha magoli 2-0 kutoka kwa JKU ya Zanzibar uwanja wa Uhuru, mashabiki povu likawatoka na siku mbili baadae, yaani jana, Simba ikafungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-1. Hapo ndio sekeseke likaanza.

Baada ya vipigo hivyo viwili kutoka kwa mapacha hao wa soka la Tanzania ambao wote wana vimo na tabia za kufanana kasoro rangi tu, nilitumia siku nzima kuwa ‘busy’ kwenye mitandao ya kijamii nikiangalia mashabiki wao watachukulia vipi vipigo hivyo vya mechi za majaribio. Na kama nilivyotarajia ni kuwa mashabiki hao wa timu zote mbili walitokwa povu la kutosha tu kila mmoja kwa wakati wake.

Nataka kukuonyesha kitu ambacho nimekishuhudia na sio kukusimulia tu japo sikuweza kuweka majina ya wahusika waliotoa maoni yao kutokana na miiko ya taaluma yangu ambayo hainiruhusu kufanya hivyo bila idhini ya mhusika.

Nimejaribu kuyaweka maoni ya mashabiki hao katika makundi kulingana na mada kuu zilizojadiliwa wengi. Ebu jionee hapa.

 

LAWAMA KWA MAKOCHA NA VIONGOZI:

1. Mwalimu muongo, ila timu iko na wigo mpana tu lakini anang’ang’ania haohao hata kwa michezo ya kirafiki. Angewachezesha lakini nafasi kubwa iwe kwa wale ambao hakuwatumia kwenye mzunguko uliopita, anataka akiumia mmoja apate kisingizio- Shabiki wa Simba

2. Ilikuwa kipimo cha mazoezi kwa mzunguko wa pili lakini mwalimu katudanganya, wangeanza ambao hakuwatumia kwenye mzunguko uliopita. Uzuri ni kikosi ambacho mwisho kilishindwa leta matokeo chanya, asipobadilika ligi itakapoanza tutalia sana.

3. Pumbav kabisa mm sijapenda ata kidogo mbona wanataka kutukosesha raha hawa viongozi wa simba lakini

 

LUFUNGA ABEBESHWA ZIGO LA LAWAMA:

1. Akicheza lufunga na mwanjali tunafungwa bora awe anapanga juko na mwanjali hapo tutakuwa salaama vinginevyo mm sjui kama tutafka hii safari

2. Kwahali hii naumbeni uongozi wetu umchezeshe banda nafasi ya LUFUNGA kwani jamaa nimzigo kwelikweli na kama hamtafanya hivyo ubingwa tusahau kwasababu huyu jamaa mechi ya yanga na aflika liyon nimakosa yake huyu sio beki wakumtegemea hata kidogo juku mnamfanyia figisufigisu lakini huyu ndoo beki kisiki hata ukiangalia mechi alizocheza juku hatujapoteza hamoja kwakwa sababu jamaa yukomakini sana mimi ninachowaomba viongozi wetu muangalie nafasi yabeki kwani beki ikiwavizuri hatambele kutakuwa vizuri mmninaimani nawashambuliaji waliopo wanauwezo wakufunga ila lufunga apumzike kwanza hiyo ndio rai yangu

 3. Lufunga Huyu C Beki Kabisaa Yaan Bora Namba 4 Acheze Banda Kuliko Huyo Lufunga Coz Jamaa Ni Mzigo Hajuw Mpira Aiseee Au Mech Nyngne Mpange Emanuel Simwanza.

4. Kama maandaliz ndo hayo na ligi yenyew inaendelea keshokutwa bc hamna ki2 mna2katisha tamaa mapema yote haya.

 

SUALA LA KIKOSI CHA PILI LAZUA UTATA:

1. Kocha huyo vip,bwana ameona ss wakufungwa sanaa anatuanzishia kikosi cha pili,naafanye mabadiliko halaka sisi hatuchezi na jku,kikosi bii,tunacheza na jku,iliyokamilika,ujinga huo,bwana je

2. Io la kusema kikosí cha pili mi sioni kama lina tija…. Kwani mazoezi si wanafanya wote kama timu moja….. Au mwalimu huwagawa na kuwafundisha A…. B. Wakiwa darasani….. Io mechi tumezidiwa kimchezo… Na tuache kulaumu kikosi B. Kwani kikosi A. Ni kipi….. Kwa upande wangu mi nimeumia….. Kuna wana yanga wenzangu eti hawaumii kwa kua ni mechi ya kilafiki… Inaingia akilini… Kwani mechi ni mechi tu…. Mbona mtani jana kashinda…. Mi ninavyo jua mechi za kirafiki ni kipimo cha kufanya vizuri sio kufanya vibaya…… Kwani mechi za kirafiki zenyewe ni mbili je zote tukipoteza itatujenga nini….. Na ninani alie omba mechi….. Kwaio tumeomba ili tufungwe ili tuangalie kikosi. Kwani kwenye ligi tunachezesha kikosi A. Au B. Au tunachezesha yanga….

Hayo ni baadhi tu ya maoni kwani ningeorodhesha maoni yote hapa basi pasingetosha.

Licha ya maneno yote hayo kutoka kwa mashabiki ambao walikuwa na hasira za kutosha kwa makocha na wachezaji wao, lakini pia hawakukosekana wale ambao walikuwa na busara ambao walikuwa wanajua malengo hasa ya walimu wao kuomba mechi za kirafiki

1. Maana ya mechi za kirafiki nikujua mapungufu yaliopo katika team kwa hiyo si kila matokeo ni kubeza wachezaji au benchi la ufundi hapana Mwalimu anaangalia muunganiko wa team ndiyo maana ata bukungu alipewa hile penalty kwani yawezekana mchezaji anaetegemewa akawa majeruhi

2. Mechi ya kirafiki imesaidia kutuoonesha tusijiamini kuongoza ligi ndio ubingwa. Hivyo kinachotakiwa ni bora kujipanga mapema kufanya marekebisho . Tunaomba UMOJA na kutathimini mchango wa wachezaji waliosaidia timu kuongoza sio kuleta wachezaji wasio na tija

3. Mashabiki bongo hatuna uvumilivu na clubs zetu…. tunapenda tuwe tunshinda tu hata friends match… bila kujali kwamba kikosi kinajaribiwa.. nimeona hii tangu juzi Yanga na JKU

4. Unajua Mimi huwa na mashaka sana na mashabiki wengine. Trial match maana yake nini? Kikosi kimejaribiwa lengo lilikuwa ni kiyabaini matatizo. Huwezi kuwaagiza wachezaji kufia uwanjani kwa mechi km hii. Unashinda then ligi inaanza wachezaji tegemeo wapo majeruhi just for trial match. Lakini mkumbuke kuwa JKU ni timu nzuri na tuliokuwa uwanjani ni mashahidi.

 Lengo la kuchukua maoni ya mashabiki na kuyaweka hapa kama yalivyo ni kutaka kuonyesha jinsi gani mashabiki walivyokuwa hawana uvumilivu kwa walimu na wachezaji wao hasa baada kupoteza mechi. Sikutaka kuhariri maoni hayo kwani ningepoteza uhalisia.

Tunajua furaha ya mpira wa miguu ni ushindi na hakuna mtu anayependa kufungwa, lakini suala la kutaka ushindi lisitufanye tusahau kuwa hizi ni mechi za kirafiki ambazo walimu huzitumia kujaribu wachezaji wao wapya waliosajiliwa au mbinu mpya za kiuchezaji hususani kwa kocha kama Lwandamina ambaye ni mgeni na hajawahi kuiongoza Yanga kwenye mchezo wowote wa kimashindano na ndio maana hata FIFA wameruhusu mechi za kirafiki kama hizi makocha kufanya mabadiliko mara nyingi zaidi hata ikiwezekana kubadili kikosi kizima kama kocha atataka.

Suala la Lwandamina au Omog kutumia wachezaji wa vikosi vya pili sio suala la ajabu na wala hakuna haja ya msingi ya kushusha kikosi cha kwanza chote wakati ni mechi ya kirafiki na wala hakuna haja ya kucheza kwa nguvu sana kwani lengo sio kutafuta pointi tatu pale bali huwa ni fursa kwa makocha kujaribu mifumo mipya na kupima uwezo wa wachezaji wao mmoja mmoja.

Kwa ujumla nilichogundua ni kuwa mashabiki wa bongo hasa wa timu hizi mbili tunaendeshwa sana na hisia. Mapenzi yanapitiliza kiasi cha kuingilia kazi za wataalamu wa benchi la ufundi. Na kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa si mashabiki tu bali hata viongozi wa timu ambao ndio tunaamini wana busara zaidi, lakini nao ni wale wale na ndio maana sioni ajabu kuona kocha kafukuzwa kwasababu ya kelele za mashabiki wanaotumia kigezo cha Mapenzi ya timu na kusahau weredi.

Ile dhana ya utani wa jadi ya mashabiki wa timu hizi mbili sio tu inaishia kwa mashabiki wa timu hizo nje ya uwanja bali sasa inaanza kuingia ndani hadi kwa viongozi na hatimaye kutupwa kwa benchi la ufundi hali ambayo inaharibu utaratibu na utulivu wa benchi la ufundi na wachezaji.

Kuna haja ya hizi mechi za kirafiki kwa hizi timu mbili kuchezwa bila mashabiki uwanjani ili wachezaji waweze kuwa huru na makocha waweze kutuliza akili zao kusoma vikosi vyao. Na ndio maana naanza kuelewa kwanini timu hizi hukimbia mji kwa ajili ya maandalizi kuelekea kwenye mechi zao za watani wa jadi.

Tuache kuwafundisha makocha kazi zao. Kila mtu ana nafasi yake kwenye timu na ndio maana huyu anaitwa kocha na huyu anaitwa shabiki. Kila mtu anaweza kuwa shabiki lakini sio kila mtu anaweza kuwa kocha. Mechi za kirafiki zisitutoe mate.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets