Menu

BURIANI AZAM FC: UNGEKUWA MWEUPE BILA HATA KUTUMIA MKOROGO; AMKA UJIPANGE, BADO UNAYO NAFASI

Na Adam Mbwana,

Hoi hoi, nderemo na vifijo vilifurika mitaa ya Chamazi nakumbukuka ilikuwa Mei 19 mwaka huu huu ambao tupo mbioni kuuaga na kuanza mwaka mwingine.

Shangwe hizo za mitaa ya Chamazi zilizoambatana na tambo za hapa na pale na kejeli za kila aina zilikuwa ni za kuwakaribisha makocha kutoka nchini Hispania ndugu Zeben Hernandez na Jonas Garcia ambao taarifa zilidai kuwa walitoka kunako klabu ya Deportivo Tenerife alipokuwa akifanya majaribio Mtanzania mwenzetu Farid Mussa ambaye juzi usiku alikwea pipa kuelekea huko kuanza maisha mapya.

Macho yangu na masikio yalikuwa ni kwenye magazeti ya michezo ya kesho yake bila kusahau huko mitandaoni ambapo nilisikia tambo nyingi sana zenye kutia moyo kama vile “Makocha wahispania kuifanya Azam kama Barcelona”, “Watatukoma”, Azam sasa kuchezeshwa tik-tak kama ya Barcelona” na nyingine nyingi, mimi kama kawaida yangu nikaishia kuguna tu nisitie neno maana waswahili wanasema ya Ngoswe muachie Ngoswe mwenyewe.

Hivi tunavyoongea nipo nasikiliza wimbo wa msanii Rich Mavoko kutoka WCB unaoitwa “Ibaki stori” huku nikikumbuka baadhi ya vionjo vinavyoimbika “…..mi na weweee, acha ibaki stori mimi na wewe….mapenzi mimi na wewe…” Nafikiri unakielewa nnachomaanisha. Ebu sasa tuwe ‘serious’ kidogo.

Juzi klabu ya Azam imetangaza kuachana na makocha wake raia wa Hispania ambao imewapa kibarua hicho miezi sita tu iliyopita kutoka mikononi mwa Mwingereza Stewart Hall. Nisiwe mnafki, kusema ukweli taarifa hizo zimenishtua sana na mwanzoni nilihisi ni tetesi tu mpaka hapo jana ambapo niliiona taarifa rasmi kutoka kwenye mtandao wa Azam kuwa ni kweli pande hizo mbili zimemwagana.

Kwa kweli tangu jana nimekuwa nikitafakari mambo mengi sana kuhusu uamuzi huo na mwelekeo mzima wa klabu ya Azam ambapo nikaamua niwashirikie mambo kadhaa yaliyopo kwenye fikra zangu. Twende sambamba…….

Hapana shaka klabu ya Azam imeleta mageuzi makubwa kwenye soka letu la ngazi za vilabu hapa nchini kwani tangu ipande kucheza ligi kuu mwaka 2009 tumeshuhudia ikivinyima usingizi vigogo vya Simba na Yanga ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikibadilishana mataji ya ligi kuu na ufalme wa soka la nchi hii. Sio siri Azam imeleta njaa kali kwa vigogo kwani kuna wengine sitaki kuwataja huu ni msimu wao wa nne wanahaha hawana hata kibakuli mkononi kama sio kikombe.

Sambamba na kuleta upinzani kwenye soka la vilabu nchini lakini naamini wakati klabu hiyo ya Azam inaanzishwa, aliyebuni wazo hilo alikuwa ana malengo mahususi kama walivyo wajasiriamali wengine wa kawaida tu. Mfano; mtu anapotaka kuanzisha biashara yoyote ni lazima awe amefanya utafiti kujua ni aina gani ya biashara afanye kulingana na uhitaji wa watu husika wa eneo hilo huku pia akiwajua fika wapinzani wake wakuu katika soko, nini wanazalisha na kwa ubora gani ili yeye aje na ubunifu zaidi ya wale waliomtangulia kwa lengo la kuliteka soko.

Naamini klabu ya Azam ilianzishwa kwa kufuata misingi hiyo ikitumia vyema makosa ya Simba na Yanga ili yenyewe iweze kuja kivingine kabisa na kisasa zaidi. Nashukuru Mungu tumeuona uwekezaji ambao Mzee Bakhresa ameufanya pale Chamazi kitu ambacho kwa miaka nenda rudi Simba na Yanga hawajawahi kufanya hadi sasa Azam wamewafumbua macho ndio wameona aibu na wao wanapigana vikumbo mjini katika jitihada za ku-copy na ku-paste.

stewart

Stewart Hall, kocha Muingereza aliyeipa Azam ubingwa wa Kagame mwaka jana

Lakini naamini Azam haikufikiria kuishia kwenye kujenga miundombinu tu, bali naamini kuna sera ambayo walijiwekea tangu mwanzo jinsi ya uendeshaji wa klabu yao na hata falsafa zao pia. Mfano sera ya klabu kama Real Madrid ni kupata mafanikio kupitia ununuaji wa wachezaji maarufu duniani kwa pesa kubwa “Galacticos”, sera ya vilabu kama Shakhtar Donestki, Benfica, FC Porto barani Ulaya ni kununua wachezaji kwa bei chee kutoka nchi zenye utajiri wa vipaji kama vile Brazil, kuwakuza wenyewe kisha kuwauza kwa vilabu vikubwa kwa pesa kubwa. Kila klabu ina sera yake ya kiuchumi na kimatokeo. Bila sera hiyo basi klabu itakuwa ni kama genge la wauza nyanya tu lisilo na muongozo, na ndio maana hata vyama vya siasa vina sera zake na nchi pia ina sera zake ambazo huwa kama MUONGOZO.

Kwa sisi hapa nyumbani kwa muda mrefu vilabu vyetu hivi viwili vya Simba na Yanga ambavyo mimi hupenda kuviita Sunche na Kapeto, vimekuwa na sera yao moja tu ya kutaka kunyamazishana na kunyimana usingizi vyenyewe kwa vyenyewe. Yaani kutambiana kununua wachezaji kutoka Rwanda na Burundi kisha wafungane kwenye mechi za watani wa jadi na ndio maana takwimu zinaonyesha kuwa makocha wa vilabu hivyo hufukuzwa kazi baada ya mechi hizo zinazowakutanisha lakini pia baadhi ya wachezaji hupata majina makubwa au kuharibikiwa majina yao kupitia mechi hizo. Shiza Kichuya na Hans Van der Pluijm watakuwa shahidi wangu namba moja.

Simba kamfungaYanga, Jangwani kumetulia, Msimbazi nderemo za kutosha, magazeti yaandike, Dar nzima ienee rangi nyekundu. Hizo ndizo sera zao na ndio maana sishangai kuona tunaboronga kimataifa kila kukicha maana sera zetu hazijalenga kimataifa. Wenye sera zilizolenga mafanikio ya kimataifa kama vile TP Mazembe, Enyimba na wengineo tumewaona. Wametukuta, wametupita na wametuacha tulipo tukitaniana kama ilivyo jadi yetu.

benchi-la-ufundi

Benchi la ufundi la Azam likiongozwa na mwalimu Zeben Hernandez na Jonas Garcia ambalo limetimuliwa hivi karibuni

Kwa kifupi nilitarajia ujio wa Azam ungeleta mapinduzi ya soka nchini sio tu katika miundo mbinu ya soka lakini pia katika sera za uendeshaji wa vilabu. Nilitegemea kuona Azam ikisema kuwa tunataka baada ya miaka kumi tuwe tumechukua kombe la Shirikisho Afrika mara mbili au tuwe tunauza wachezaji tuliowakuza nje ya nchi kwa pesa kubwa, lakini cha kusikitisha ni kuwa huu ni mwaka wa nane Azam inafikisha bado sijaona sera yao wanayoisimamia ambayo ndio inaongoza klabu. Kwa kifupi niseme kuwa Azam wamepoteza mwelekeo.

Naweza kusema Azam wamepoteza mwelekeo kwasababu moja kubwa. Azam inataka kushindana na Simba na Yanga kuliteka soko la mpira wa miguu Tanzania na kuwafanya watanzania wasahau kuhusu Simba na Yanga kisha wahamie Azam. Japo hawajawahi kusema hivyo wazi wazi lakini matendo yao yanasadifu kauli hii.

Kutaka kushindana na Simba na Yanga ndio kosa kubwa Azam wanalolifanya huku wakishindwa kukumbuka kuwa vilabu hivi ni vya urithi kwa mamilioni ya watanzania na sio rahisi kuwatoa huko kwani kwao ni kama dini.

We unafikiri kwa mtu mzima kama Steve kutokwa machozi uwanjani baada ya Okwi kumgeuza geuza Nsajigwa kama Chapati tena mbele ya Kamera alipenda? Yale ni mapenzi. We unafikiri mashabiki kuzimia uwanjani kisa Simba kafungwa na Yanga au kinyume chake huwa ni jambo la kawaida? We unafikiri mashabiki wa Simba kun’goa viti uwanjani kisa mwamuzi kakubali goli la Tambwe la mkono ni jambo la kawaida? Sio kawaida hata kidogo kwasababu Simba na Yanga ni moja wapo ya dini za Watanzania walio wengi. Halafu wewe uje leo tu uwabadilishe kizembezembe hivyo?

Azam walitakiwa washikilie sera yao ileile ya mapinduzi ya soka Tanzania, sera ambayo ilitakiwa ionekane kwa vitendo na sio kwa maneno tu. Azam kama mwanamapinduzi alitakiwa asiruhusu kabisa siasa za Simba na Yanga ziivuruge hata kidogo kwani wameshaona kwa muda mrefu na wanajua madhara ya siasa kwenye soka.

joseph

Kocha Joseph Omog aliyewapa Azam ubingwa wa kwanza wa VPL

Kumfukuza kocha uliyempa kibarua kwa miezi sita tu eti kwa kisingizio cha matokeo mabovu ni siasa iliyopitiliza. Aliyesema kuwa makocha ni waganga wa kienyeji wanaoweza kukupa matokeo uyatakayo hapohapo ni nani? Labda kama Freemason wameshaingia kwenye soka.

Zeben wakati anasaini mkataba aliomba kupewa muda ili ajenge timu yenye kuleta ushindani kimataifa, timu ambayo ndani ya miaka kadhaa itaweza kutunishiana misuli na kina Al Ahly na TP Mazembe ambao ndugu zao Simba na Yanga wamewashindwa kwa miaka nenda rudi, na wala hakusema kuwa anataka kuipa Azam ubingwa wa VPL msimu wa 2016/17.

Sasa kwanini umtimue wakati unamletea wachezaji wa majaribio wiki mbili kabla ya kuanza kwa ligi?, kwanini umtimue wakati umemjazia wachezaji kibao ambao hawahitaji na wala hawaendani na mfumo wake, wachezaji ambao asingeweza kuwatimua wote ndani ya msimu mmoja bali angeendelea kuwapunguza mmoja mmoja na kuingiza wengine awatakao yeye wenye tija? HIYO NI SIASA ILIYOPITILIZA.

Naomba nimalize kwa kuushauri uongozi wa juu wa Azam japo naweza kuonekana kuwa sina akili, lakini ningependa kuwaambia kuwa ifike kipindi wajue wanataka nini katika soka, Wajue wanataka kupata mafanikio kupitia sekta ipi kwenye soka kwani soka ni pana. Wakiendelea kuvurugwa na wimbi la Simba na Yanga basi hawana muda mrefu watapoteana.

watatu

Wachezaji wapya kutoka Ghana wakisani kuichezea kwenye dirisha hili dogo la usajili mbele ya mwalimu Zeben

Kama wanazalisha vipaji ili waje kuvitumia ndani ya miaka kumi basi wawe wavumilivu kwani kila sera ina faida na hasara zake na uzuri ni kuwa hawana presha ya mashabiki wanaotaka mafanikio kwa pupa kama wa Simba na Yanga. Watulize akili chini watafakari na wajue wanachokitaka na sio kutaka kujifananisha na Simba na Yanga, wao waje kivyao na kwa ubunifu wao. Na kama wanataka kumwaga pesa kununua wachezaji wa kuwapa kombe la CAF basi wajitose kama mwenzao Moise Katumbi na sio kununua wachezaji wa mafungu kutoka Afrika Mashariki na kisha kutuaminisha kuwa hao ndio Reinford Kalaba au Stopila Sunzu.

Uswahili ni jadi yetu Watanzania lakini kama Azam wakitaka kutusua, basi waache uswahili wafate weredi na waache kutembelea nyota za watu ambazo hazijulikani kama bado zinang’aa au zimeshafifia.

Nawasilisha…!!!!

 

adammbwana3@gmail.com

0682 502639/0762989979

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets