Menu

KUMTWIKA MOURINHO ZIGO LA LUKAKU NA DE BRUYNE NI KUMUONEA TU; CHELSEA WANA SIRI NZITO KATIKA HILI

 Na Adam Mbwana,

Kwa muda mrefu sasa mashabiki wa soka duniani wamekuwa wakihoji kitendo cha klabu ya Chelsea kuwa na wachezaji wengi vijana kwa mkopo bila ya kuwapa nafasi kwenye kikosi chao cha kwanza ili waweze kutumikia. Sikuwahi kushangaa kutokana na hoja hizo kwani nilijua fika hakuna jambo linalofanyika bila ya watu kuhoji kutokana na ukweli kwamba sio kila mtu anaweza kujua nini umemaanisha unapotaka au unapoanza kufanya jambo Fulani kwahiyo ni halali yao kuhoji.

Licha ya kutowahi kusukukwa kuandika kuhusu mikopo hiyo ya wachezaji wa Chelsea, lakini wiki iliyopita uzalendo ulinishinda kidogo pale kwenye pitapita zangu huku na kule nikamsikia Profesa Wenger akilalamikia vilabu vyenye tabia ya kutoa wachezaji kwa mkopo bila ya kuwapa nafasi kwa malengo ya kujinufaisha wao wenyewe kwa mauzo ya wachezaji hao. Katika hali ya kawaida Wenger alikuwa haisemi Chelsea, lakini kwasasa hata sisimizi tu ambaye hafatilii soka anajua kuwa Chelsea ndio mlengwa mkubwa wa vijembe vile vya Wenger. Kwa taarifa yako tu ni kuwa Chelsea ina wachezaji 30 vijana waliotolewa kwa mkopo kwenye vilabu vingine barani Ulaya.

chelsea-game2

Sasa ebu tutazame kwanini Chelsea wamekuwa wakopeshaji maarufu barani Ulaya halafu tutarudi kwenye mada yetu kuu ya leo.

Mwaka 2010, Bodi inayoongoza Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA), iliweka utaratibu mpya uliopewa jina la Financial Fair Play (FFP) ili kuleta nidhamu na usawa katika matumizi ya fedha kwa vilabu vya soka barani humo.

Iliilazimu UEFA kufanya hivyo kufuatia baadhi ya vilabu kuwa na matumizi makubwa mno ya pesa hasa katika manunuzi ya wachezaji hali ambayo ililalamikiwa na baadhi ya makocha wa vilabu visivyo na uwezo mkubwa wa kifedha kuwa inahatarisha ushindani katika soka kwani vilabu vyenye fedha kama vile Real Madrid vitakuwa havishikiki. Huku pia tusisahau kuwa miongoni mwa makocha waliowahi kulalamika kuhusu usajili wa kufuru alikuwa ni Wenger huyo huyo japokuwa huwezi kusema Arsenal haina hela.

Financial Fair Play (FFP) ilichofanya ni kuvilazimu vilabu kutumia pesa viliyoitengeneza vyenyewe na sio kukopa pesa kwenye mabenki makubwa na kufanya usajili wa kufuru au kutumia mabilioni ya wamiliki wa timu zao kufanyia kufuru za usajili. Hivyo basi, kama umeingiza Sh 100 kwa mwaka, usajili wako usizidi Sh 100 lasivyo utapewa adhabu kwa kuvunja masharti.

Bila shaka kwa masharti hayo utaona vilabu mbalimbali vilianza kukuna vichwa kutafuta njia mbadala ya kuwaingizia kipato kikubwa ili waendelee kufanya matanuzi. Kuna walioongeza bei za viingilio vya uwanjani, kuna walioongeza bei za jezi, kuna walioboresha mikataba yao na makampuni makubwa ilimradi tu kila mmoja aongeze kipato chake.

Kwa klabu ya Chelsea ambayo moja kwa moja iiliguswa na FFP, nayo haikuwa nyuma katika suala zima la kutafuta mbinu mbadala za kutunisha mifuko yake kwani hapo awali pesa za Abramovch zilikuwa zikiwatia kibuli na katika kufikiria hapa na pale, Chelsea sasa ikaamua kuwa madalali ambapo huchukua wachezaji vijana wenye vipaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa bei chee na kuwatoa kwa mkopo kisha baadae kuwauza kwa bei kubwa wakishakomaa au kuwatumia kama chambo ya kunasia wachezaji wengine.

emenalo

Michael Emanalo, Mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea

Hapo ndipo hoja zilianza kuibuka kwani tofauti na matarajio ya wengi, Chelsea haikuwa ikifanya hivyo ili kukuza wachezaji watakaowatumia kwenye timu yao ya wakubwa siku za usoni bali ilikuwa ikifanya hivyo ikiwa ni sehemu ya biashara. Hivyo hapo uelewa ulitofautiana.

Moja ya wachezaji waliozua gumzo kubwa kufuatia utaratibu huo ni pamoja na Kevin de Bruyne ambaye alisajiliwa kutokea Genk ya Ubelgiji alipo Mbwana Samatta kwa dau la paundi milioni 7 mwaka 2012 huku wengi wakiamini kwa kipaji chake basi Mbelgiji huyo angeweza kutusua hadi kikosi cha kwanza lakini aliishia kutolewa kwa mkopo na mwishowe kuangukia Wolfuburg kwa paundi milioni 18. Na sasa yupo Man City akiwa ni mwiba mkali kila mtu akimlaumu Mourinho kwa kumruhusu nyota huyo aondoke. Kosa si la Mourinho jamani.

Mwingine ni Romelo Lukaku ambaye alinunuliwa mwaka 2011 kutokea Anderlecht ya Ubelgiji kwa ada ya paundi milioni 10 huku wengi wakiamini huyo ndiye Drogba mpya. Lukaku aliishia kwenda West Brom na Everton kwa mkopo kabla ya kuuzwa moja kwa moja kwa dau la paundi milioni 28. Licha ya Chelsea kupiga pesa yao ndefu lakini bado watu wameendelea kumkalia kooni Mourinho kwa kuruhusu kijana huyo aondoke ambaye kwa sasa ni mwiba wa kuotea mbali akiwa na Everton.

mou

Jose Mourinho na Romelo Lukaku wakiwa Chelsea msimu wa 2013-14

Unamkumbuka Oriol Romeu kutokea Barcelona mwaka 2011 wengi wakiamini ndiye Michael Ballack mpya, lakini kaishia kuuzwa Southampton, unamkumbuka Matic aliyesajiliwa mwaka 2009 akakosa namba na msimu uliofuata akapelekwa Benfica akiwa ni sehemu ya dili ya kumnunua David Luiz halafu miaka minne baadae Mourinho akamrudisha kwa paundi milioni 21?

Yaani ni wengi sana nikianza kuwataja hawataisha na wengine bado wapo kwenye mkopo wanasota nao, watu kama vile Mario Pasalic, Kenedy, Mark Van Ginkel, Lucas Piazon, Christian Cuevas, Gaely Kakuta, Christian Atsu, Nathan Ake , Patrick Bamford na wengine wengi huku nikiwaona watu kama vile Ruben Loftus Cheek, Nathaniel Chalobah na Ola Aina mkopo ukiwaita mwishoni mwa msimu huu.

Kwa kifupi tu ni kuwa Chelsea wanachokifanya sio kama ni bahati mbaya. Wengi wanamlaumu mkurugenzi wa ufundi Michael Emenalo kwa kufanya biashara kichaa, lakini ukweli ni kuwa si biashara kichaa kwani anajua anachokifanya.

Klabu ya Chelsea sio klabu ya kukuza vipaji kwa kuvipa nafasi kikosi cha kwanza kama wafanyavyo Benfica, FC Porto, Shakhtar Donetski na wengine wengi. Wanaponunua wachezaji wadogo si kwasababu wana lengo la kuwakuza na kuwapandisha, Lahasha! Bali huwatoa kwa mkopo hadi pale watakapokomaa kiuchezaji na kuwauza kwa dau zuri au kuwatumia kama chambo ya usajili.

Ni wachache sana wameweza kutusua kikosi cha kwanza cha Chelsea kutokea kwenye utaratibu huu, mtu kama Victor Moses alivumilia, akaenda kwa mkopo na kupata uzoefu hadi pale Conte alipomuona anafaa. Mtu kama Thibaut Courtois alienda Atletico Madrid akaonyesha uwezo mkubwa sana katika umri wake mdogo kiasi cha Mourinho kuona kuna umuhimu wa kumtumia badala ya mkongwe Petr Cech na akaweza kuipa Chelsea ubingwa wa EPL katika msimu wake wa kwanza tu. Ni nadra sana, inapotokea basi huwa kibahati bahati lakini hayo si malengo ya awali ya utaratibu huu wa Chelsea.

Chelsea ni klabu inayowinda makombe kila msimu na hiyo ndiyo sera yake. Haiwezi kuwaamini vijana wadogo na kuwapa nafasi kikosi cha kwanza wacheze na timu kama Liverpool au Man City. Hawako tayari kujitoa mhanga kiasi hicho na ndio maana wapo radhi kutoa kitita kikubwa kumsajili Marco Verrati wakati Loftus Cheek yupo pale.

loftus

Ruben Loftus-Cheek

Wenger analijua hilo lakini amekuwa akibisha kutokana na yeye kuwa na mtazamo tofauti katika soka kwani yeye falsafa yake ni kuwapa nafasi wachezaji vijana kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal bila kujali atatwaa kombe mwisho wa siku au la…na kwa miaka zaidi ya kumi hajawahi kutwaa kombe la EPL kwasababu ya falsafa yake hiyo hadi watu kama Man City wamekuja wamefungua pochi wakawachukua kina Silva na kubeba nao mataji yeye yupo palepale.

Tumewaona Van Persie, Fabregas, Clichy, Nasri, Adebayor, Henry, Song, Ramsey, Vela, Rosicky, Toure, Eboue wakipitia kwenye mikono ya Wenger baada ya kuwapa nafasi kikosi cha kwanza licha ya umri wao mdogo kipindi hicho na wakati wakiwa wameshakomaa tayari kwa kulipa fadhila, hutaka kuondoka kitu kinachomlazimu Wenger kuwauza. Hakuna aliyewahi kumgusa Wenger kwasababu hiyo na mpaka sasa yupo palepale akiendelea kuwakomaza kina Fransic Coquelin, Nacho Monreal na Iwobi wake na wala hajafukuzwa. Lakini angekuwa Chelsea asingechukua hata misimu miwili angekuwa kashatimuliwa.

Tuongee ukweli na tuache unafki, Hivi wakati Matic anatua Chelsea mwaka 2009 kukiwa na rundo la viungo kama vile Michael Ballack, Frank Lampard, Michael Essien, Obi Mikel, na Deco angepata nafasi kweli? Wakati De Bruyne anakuja Chelsea mwaka 2012 kukiwa na watu kama Oscar, Hazard, Mata, Schurrle, Ramires, angeweza kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara kweli? Suala la mchezaji kuwa mtamu baada ya kupata timu nje ni kawaida na wala hapaswi kulaumiwa aliyemuuza kwani huenda kwa wakati aliokuwepo, waliokuwepo bora zaidi yake.

nemanja

Nemanja Matic aliposajiliwa Chelsea msimu wa 2009-10

Mwisho kabisa,

Wenger yuko sahihi kuwa vijana wanatakiwa kupewa nafasi kwenye timu ya wakubwa ili kukua na kuwa msaada siku za usoni. Lakini hilo huambatana na uvumilivu wa mwenye mamlaka ya mwisho ya klabu. Mabosi wa Arsenal si sawa na bosi wa Chelsea katika suala zima la uvumilivu na ndio maana yeye bado anadunda.

Na pia, suala la De Bruyne na Lukaku lisiwe kama fimbo ya kuuchapia mfumo wa Mkopo wa klabu ya Chelsea kwani, wanaposajiliwa wachezaji vijana klabuni pale lengo la kwanza kabisa sio kuwapa nafasi kwenye kikosi cha kwanza bali ni kuwatoa kwa mkopo na wakishakomaa kuwauza ili kupata pesa au kuwajumuisha kwenye sehemu ya dili la kumnasa mchezaji fulani mkubwa na ikitokea mmoja akatusua kikosi cha kwanza basi huwa ni kama muembe kuota kwenye mchongoma.

Ukiangalia kwa karne ya sasa, Usajili ndio huvigharimu vilabu mabilioni ya pesa kuanzia kwenye ada za uhamisho hadi mishahara. Hivyo Chelsea wamemua kupunguza gharama kwa mfumo wao huu aidha kwa kumuuza mchezaji aliyekomaa angalau kwa dau kubwa au kumtumia kama sehemu ya kumnasia mchezaji mwingine mkubwa.

Kila mtu na sera yake bwana….!!!! Wewe ukichinja wenzio wananyonga.

 

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets