Menu

PAUNDI MILIONI 773 ZILIKUWA BENCHI: “NI KWELI VIGOGO UINGEREZA VIMEIDHARAU FA CUP WIKIENDI HII?

Na Adam Mbwana,

Vilabu mbalimbali vya Ligi Kuu nchini Uingereza mwishoni mwa wiki kwa pamoja vimetajwa kuishusha hadhi ya Kombe la FA ambalo ni kombe kongwe zaidi duniani baada ya kuwaweka benchi wachezaji wake wenye thamani ya jumla ya paundi milioni zinazokaribia kufikia 800 huku zile klabu zinazoshika nafasi sita za juu kwenye msimamo wa EPL pekee zikiwaweka benchi wachezaji wake wenye thamani inayofikia paundi milioni 521.3

Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa na mwandishi Ian Baker wa tovuti maarufu ya michezo duniani ya The Sun inadai kuwa Manchester United ndio imeonekana kuwa na dharau zilizopitiliza baada ya kuwaweka benchi wachezaji wake wenye thamani ya paundi milioni 150 wakiongoza na Pogba (Paundi m89) Henrick Mikhitaryan (paundi m30) pamoja na wengine kama vile Juan Mata na wengine ambao kwa pamoja wanafikia thamani hiyo ya paundi milioni 150. United iliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Reading.

man-u

Wachezaji wa Manchester United wakishangilia ushindi dhidi ya Playmouth

Liverpool nao waliweza kuonyesha dharau zao za waziwazi kwa kuwaweka benchi wachezaji wao wenye thamani ya paundi milioni 117 kama vile Adam Lallana, Giorginio Wijnaldum na Roberto Firminho huku kocha Jurgen Klopp alisikika akisema kuwa lilikuwa ni benchi bora kuwahi kutokea kwenye maisha yake ya soka akimaanisha kuwa hajawahi kuwaweka benchi wachezaji wenye majina na thamani kubwa kama alivyofanya jana tangu aanze kufundisha soka licha ya kutoa sare ya 0-0 na vibonde Plymouth.

liverpool

Moja ya matukio kwenye mchezo wa jana kati ya Liverpool dhidi ya Playmouth iliyoisha kwa sare ya 0-0 uwanja wa Anfield

Chelsea nayo iliwapunzisha nyota wake kama Vile Diego Costa, Eden Hazard, David Luiz na wengineo ambao thamani yao inafikia jumla ya paundi milioni 110 wakifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Peterborough .

chelsea

Wachezaji wa Chelsea wakishangilia moja ya mabao kwenye mechi dhidi ya Peterborough hapo jana

Man City ikiwaweka benchi nyota wake kama vile Jesus Navas, Kolarov, Claudio Bravo pamoja na wengine ambao jumla wana thamani ya paundi milioni 88.8 huku wakiibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya West Ham.

Ukweli ni kwamba vilabu vingi vya Uingereza hulitumia kombe la FA na kombe la Ligi kama sehemu ya kuwapa nafasi wachezaji wao ambao wamekuwa hawapati nafasi mara kwa mara kwenye mechi za ligi kuu huku ikiwapumzika nyota wao wenye majina makubwa kwa ajili ya mechi za ligi Kuu.

Katika hatua hizi za mwanzoni za kombe la FA makocha hawapo tayari kuona wachezaji wao nyota wakipata majeraha yasiyo ya lazima kwani wanawaandaa kwa ajili ya mikikimikiki ya Ligi kuu ambayo ndiyo yenye maana zaidi kwao huku wakianza kuwatumia nyota wao hao kuanzia kwenye hatua za robo fainali ya mashindano na kuendelea hadi fainali.

kombe-la-fa

Kombe la FA

Kila mtu anaweza kuwa na maoni yake tofauti juu ya hili lakini swali la msingi ni kuwa wewe kama ungekuwa Meneja wa Manchester United ungependa kuona wachezaji wako muhimu kama vile Zlatan Ibrahimovich, Paul Pogba na Henrikh Mikhitaryan wakipata majeraha kwenye mechi ya FA dhidi ya Reading wakati siku ya jumapili ya wiki inayofuata una mechi nzito ya Ligi kuu dhidi ya Liverpool ambayo huenda ikaamua hatma yako ya kuingia top 4?

Huwa ni nzuri timu ikishinda ikiwa haina wachezaji wake tegemeo kwani huonyesha ni jinsi gani hadi wachezaji wa benchi ni wazuri pia na ndio hapa tunapopata kuona tofauti kati ya timu kubwa na ndogo.

Kama Chelsea imeweza kuwatumia kina Ruben Loftus-Cheek, Nathan Chalobah, Asmir Begovic na wakapata ushindi mnono dhidi ya Peterborough ambayo ‘ilivunja kabati’ ina maana kuwa wachezaji wa benchi wa Chelsea ni bora zaidi kuliko wale wa kikosi cha kwanza wa Peterborough.

Sitaki kusema kuwa thamani ya Kombe la FA ambalo ndilo kombe kongwe zaidi duniani imeshushwa wikiendi hii kama Ian Baker anavyosema, kwa kuwa hata ukiangalia orodha ya timu zinazoongoza kwa kulitwaa kombe hilo mara nyingi ni zilezile kubwa.

orodha

Orodha ya timu zinazoongoza kwa kutwaa kombe la FA mara nyingi zaidi

Vilabu vikubwa kama vile Chelsea, United, City, Arsenal na Liverpool huanzia raundi ya 3 ya michuano hii ambayo huwa na jumla ya timu 64 hivyo uwezekano wa kukutana na timu za daraja la pili ni kubwa sana kwenye hatua hiyo na ndio maana kunakuwa hakuna haja ya kutumia nyundo kuua mende, lakini inapofika hatua ya robo fainali utaona hata upangaji wa vikosi hubadilika kwani utaona kocha anashusha ‘full mkoko’ kwasababu katika hatua hiyo wanabaki wababe tupu ambao wana uchu wa makombe na sio wale wasindikizaji wa raundi ya tatu.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets