Menu

KARIBU ARISTICA CIOABA: NASIKIA UMEYAZOEA ‘MALARIA’ YA AFRIKA; BASI HAPA KWETU KUNA ‘MALARIA’ NA ‘UKIMWI’

Na Adam Mbwana.

“Najua Azam FC hapa Tanzania ni moja ya timu kubwa yenye historia huko nyuma, napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuja kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri.” Aristica Cioaba

Tuanze kwa kauli hiyo ya kocha mpya wa Azam kutoka nchini Romania, Aristica Cioaba ambaye hivi juzi tarehe 10 ya mwezi huu wenye historia ya urefu usioisha haraka, alimwaga wino kuashiria kuingia mzigoni kwa mkataba wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezwa endapo kama wataridhika nae. Sina tatizo na kauli yake hiyo kocha Aristica kwani ni kawaida kwa kocha yeyote anapoanza kibarua kipya kutoa hotuba yenye mvuto

Aristica mwenye umri wa miaka 45 anajitosa kurithi mikoba ya Zeben Hernandez ambaye alitimuliwa mwezi uliopita ikiwa ni miezi takribani sita tu akiwa amesaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo yeye na jopo lake kutoka Hispania, lakini nakumbuka wakati nae akitwaa mikoba ya kuifundisha Azam kutoka kwa Stewart Hall alitoa hotuba nzuri pia.

“Malengo yetu ni kuifanya Azam kuwa na mfumo mpya wa soka la kisasa kuanzia utambulisho kama timu, mbinu zetu za kufanya kazi na pia katika mechi…Kwangu mimi na mwenzangu kufanya kazi Afrika ni uzoefu mzuri na tunafuraha sana,” Hayo yalikuwa maneno ya kutia moyo kutoka kwa Zeben Hernandez.

Ukiangalia hotuba hizo za kutia moyo kutoka kwa makocha wawili wa kigeni walipokuwa wanatambulishwa, utagundua kuwa zinafanana lakini kuna kitu kimoja ambacho ni tofauti. Kuna mmoja ndio kwanza alikuwa anaonja radha ya Afrika kwa mara ya kwanza na kuna mwingine tayari ameshaionja radha hiyo.

Zeben alikuwa mgeni kabisa kwenye soka la Afrika hususani Tanzania ambayo anadai aliijua kupitia Farid Mussa aliyekwenda klabu ya Tenerife kwa majaribio wakati huo yeye akiwa anafanya kazi klabuni hapo huku Aristica yeye kashaionja radha ya Afrika japo sio Tanzania kwani kashawahi kuvifundisha vilabu vya Morocco, Ghana na Misri, nchi ambazo zipo juu ya Tanzania kisoka.

karistica

Aristica Cioaba, Kocha mpya wa Azam FC

Kikubwa nnachojaribu kuzungumzia hapa ni msaada wa uzoefu wa soka la Afrika kwa vilabu vya Tanzania ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikihangaika kujikwamua kutoka kwenye wimbi la ufinyu wa mawazo na umasikini na mafanikio kimataifa.

Ni jambo jema kumuona kocha akija kufundisha Tanzania huku akiwa na uzoefu wa kufundisha Afrika kwani inakuwa ni rahisi sana kwake kuzoea mazingira kijiografia na kisaikolojia maana ukweli ni kwamba soka la Afrika ni tofauti na Ulaya au sehemu nyingine za dunia na ndio maana halitakuwa jambo la kushangaza kumuona Pluijm akiiongoza klabu ya Afrika kutwaa CAF Champions League kuliko mzungu aliyetokea Ulaya moja kwa moja hata awe Mourinho. Labda kama mzungu huyo atakuja kufundisha klabu kama vile Al Ahly au TP Mazembe ambazo zimejaa uzungu mwingi kuliko uswahili ambao ndio jadi yetu.

Kufundisha soka Afrika ni pasua kichwa na inahitaji moyo wa ziada kuweza kuendana na mazingira. Kufundisha soka Afrika yenye vilabu vyenye wapiga pesa kibao tena wakiwa katika ngazi za juu za uongozi sio jambo rahisi, soka ambalo linaamini katika uchawi ili kupata matokeo kuliko mazoezi na lishe bora kwa wachezaji.

Achana na matatizo hayo ya Afrika ambayo unaweza kuyaona makubwa yaliyoshindikana, kwani licha ya uwepo wake lakini bado vilabu kama vile Enyimba, Zesco, Raja Casablanca, Asante Kotoko vinafanya vizuri kwenye mashindano ya ngazi ya vilabu. Kweli kwenye nchi ya vipofu, chongo ndiye mfalme.

Matatizo ya soka la Afrika yanajulikana na yapo kwenye kila nchi ingawa yanatofautiana kwa uzito wake na ndio maana leo hii Cameroon ni bora mara mia moja ya Tanzania ingawa Cameroon hiyohiyo ikikutana na Hispania inakuwa nyanya.

Sina uhakika kama kocha mwenye CV nzuri ya kuzifundisha klabu kubwa Afrika na kuzipa mafanikio anaweza pia kufanya vizuri akiwa na vilabu vya Tanzania. Anaweza kufurukuta kwenye ligi yetu ya hapa nyumbani lakini kimataifa asiweze kufua dafu mbele ya wababe wa bara hili.

Ingawa Afrika ina matatizo lakini nahisi matatizo ya Tanzania yamezidi, tena kwa asilimia kubwa na ndio maana sisi sio kama Cameroon au Nigeria japokuwa wote hali zetu sio nzuri.

Kuna kocha aliyewahi kuja kufundisha klabu ya Tanzania akiwa na CV nzuri kama Joseph Omog? Omog alikuja kuifundisha Azam mwaka 2013 akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.

joseph omog

Kocha Joseph Omog wakati akiifundisha Azam

Kadhalika mwaka huo wa 2013 akisaini Azam, Omog alitoka kuiongoza klabu hiyo ya A.C Leopard kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Lakini baada ya kuja Azam na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kama alivyofanya akiwa na A.C Leopard, nini ilikuwa hatma yake ndani ya Azam? Aliishia kutimuliwa.

Mkumbuke Hans Van der Pluijm alikuja kuifundisha Yanga akiwa na uzoefu wa kufundisha vilabu vikubwa vya Afrika kama vile Ashanti Gold, Berekum Chelsea na Medeama vya nchini Ghana na akaweza kufanya makubwa. Amekuja Yanga na kuifikisha hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini nini kilifuata? Aliishia kutimuliwa

Mkumbuke Zdravko Logarusic ambaye wakati anakuja Simba mwaka 2013 alikuwa ametoa kufundisha klabu kubwa ya Ashanti Gold ya Ghana ambayo ni miongoni mwa klabu kubwa barani Afrika lakini uzoefu wake huo uliweza kuinufaisha Simba kimataifa? Jibu ni hapana.

Siku hizi ishakuwa kama fashion kwa vilabu vya Tanzania kuchukua makocha wenye uzoefu wa kufundisha Afrika kwa madai kuwa wanaweza kuhimili, ni kweli wanaweza kuhimili kwasababu washafundishwa uswahili uswahili wetu.

Hata hivyo sio jambo baya, lakini je, uzoefu wao huo umeweza kuvisaidiaje vilabu vyetu hapa nyumbani hususani katika michuano ya kimataifa? Hujiulizi tu swali kuwa kwanini hapa kwetu haiwezekani? Kama iliwezekana kwa Omog akiwa na A.C Leopards ya Congo ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa ya kawaida sana kwanini alishindwa Azam?

Lazima tukubaliane kuwa hii ndio Tanzania bwana, Tanzania ambayo viongozi wa vilabu ndio wanasajili wachezaji bila kushirikisha makocha. Hii ndio Tanzania yenye mashabiki wa soka ambao wote wanaweza kuwa makocha na utaujua ufundi wao pindi timu ikifungwa. Hii ndio Tanzania yenye viongozi wa soka wanaompangia kocha kikosi cha kuanza kwenye mechi na hii ndiyo Tanzania ambayo kibarua cha kocha kinategemea mechi ya Simba na Yanga.

Sioni sababu ya kushangaa kwanini hatufanyi vizuri kimataifa wakati uozo uliopo ni wa kiwango cha juu ambacho hata shetani wa soka angeshangaa kuusikia. Uozo ambao sio kama hatuujui, ila tunaamua kuulea kwasababu ndio tumeukuta.

Ni lazima tukubaliane kuwa Soka la Tanzania halitaweza kuendelea hata aje Mourinho kufundisha Simba au Wenger kufundisha Yanga kwasababu mara nyingi tu tumeshaona kuwa tatizo sio makosha, tatizo ni mfumo wa soka letu katika ngazi za juu kabisa za uongozi na ndio maana sitishikagi na kauli za makocha wa kizungu wanaokuja kwa mbwembwe wakijinadi kuwa wanalijua vyema soka la Afrika.

Mwambieni Aristica Cioaba kuwa hii sio Afrika aliyoizoea yeye ambayo matatizo yake ni ya kawaida. Mwambieni kuwa hii ni Tanzania. Japokuwa Tanzania ipo Afrika lakini matatizo yake ni ya kiwango cha juu.

Mwambieni kuwa Malaria inaongoza kwa kuua watu wengi Afrika lakini haitishi kama Ukimwi. Matatizo ya huko Afrika alikowahi kufundisha ni ya kawaida tu kama Malaria na yanatibika lakini huku kwetu Tanzania ambako hapafanani na Afrika matatizo yetu hayatibiki sanasana huwa tunajaribu kuyapunguza makali kama ilivyo kwa Ukimwi.

Kale katabia ketu ka kufukuza makocha kataendelea kututesa sana tu kwani shida sio makocha bali ni mfumo. Kocha hata atoke TP Mazembe aje Tanzania lakini bado tutaboronga tu maana hatuna tofauti na mtu aliyekiri kuacha dhambi na kumrudia Mungu wakati nyumbani kwake amejaza kreti za pombe kali.

Soka la Afrika lina matatizo, ukifanikiwa kuyatatua usijisifie kwani bado hujafika Tanzania. Ukiweza kuyatatua na haya yetu basi jina lako halina budi kuandikwa kwa wino wa dhahabu.

Karibu Aristica Cioaba. Hii ndio Tanzania.

Comments

comments

Please follow & like us

Video

Tweets