Kuelekea mechi sita za mwisho za ligi ya Vodacom, kocha wa Yanga George Lwandamina amesema anauhakika wa ubingwa licha ya kuandamwa na majeruhi wengi msimu huu.

Lwandamina amesema kuwa anataka kuwajenga vizuri wachezaji waliopo kwa lengo la kuhakikisha wanabadilika na kuisaidia timu hiyo iweze kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

“Ni kweli tunao wachezaji wengi muhimu majeruhi lakini hilo halina shida wapo vijana ambao nimewajenga kipindi hiki cha mapumziko naamini watafanya vizuri na kutetea ubingwa wetu,” amesema Lwandamina.

Kocha huyo raia wa Zambia amesema anatarajia kulionyesha hilo kwenye mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Azam na hiyo inatokana na Donald Ngoma na Amissi Tambwe kuwa na hatihati ya kutocheza.

Amesema Yanga ina kikosi kipana ispokuwa kinachowasumbua kwasasa ni wachezaji hao kutoaminiwa na hivyo kujitoa katika majukumu ya kuipigania timu yao na kuonekana hawana msaada.

Amesema kama kocha amejitahidi kuwarudisha kwenye hali yao ya kawaida wachezaji hao na anajivunia kwakua wanauwezo mkubwa ispokuwa wwalipoteza ari ya kujituma kutokana na kukatishwa tama na kocha aliyekuwepo kutokana na kuwekwa benchi muda mrefu.

“Wataonyesha maajabu yupo Matheo Anthon, Malimi Busungu na wengine ambao hawajazoeleka kuanza kikosi cha kwanza naamini watu wasubiri kuona mambo kuanzia Jumamosi kwenye mchezo wetu na Azam FC,” amesema.

Yanga inayokabiliwa na kibarua kigumu cha kuwakabili MC Alger kwenye mchezo wa kufuzu hatua ya Makundi ya michuano ya Kombe laShirikisho Afrika inaendelea na mazoezi yake kwenye uwanja wa Polisi Dar es Salaam.